Mtoto adaiwa kuuawa kwa jirani alikokwenda kucheza

Moshi. Mtoto wa miaka mitatu na nusu, Ivan Chuwa ameuawa kwa kukatwa shingo, mtuhumiwa akidaiwa kuwa ni kijana jirani yao kutokana na imani za kishirikina.

Tukio hilo lililotokea jana Agosti 15, 2025 saa 10:00 jioni, wakati mtoto huyo akicheza kwa jirani, limezua taharuki miongoni mwa wanajamii.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha tukio hilo lililotokea katika Kijiji cha Manushi Ndoo, wilayani Moshi.

Amesema polisi linawashikilia watuhumiwa wawili ambao ni Bahati Kiria na Severina Mafoi (mganga wa kienyeji). Wote ni wakazi wa Kijiji cha Manushi Ndoo.

“Mtuhumiwa Bahati Kiria inadaiwa alitenda uhalifu huo baada ya kwenda kwa mganga wa kienyeji Severina Mafoi akitaka apewe dawa za kumfanya apate utajiri. Inadaiwa alielezwa na mganga huyo akitaka kupata utajiri auwe mtoto mdogo ndipo akaenda kutekeleza kwa kumuua mtoto wa jirani yake,” amesema.

Kamanda Maigwa amesema uchunguzi unaendelea na utakapokamilika hatua zingine za kisheria zitachukuliwa.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava amesema: “Mtoto ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali shingoni na mtu anayeitwa Bahati Kiria ambaye ni mfanyabiashara. Kiini cha tukio hili ni imani za kishirikina, mtuhumiwa alikuwa akiamini kuwa atapata utajiri kwa kumtoa uhai huyu mtoto.”

Amedai: “Alimvizia mtoto huyu akiwa anacheza akamchukua akaenda naye shambani kisha akamkata shingo. Kwa nadharia ya tukio lilivyo anaonekana alichinjwa. Kijana huyo amekamatwa na anaendelea kushikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi na mwili wa mtoto umehifadhiwa Hospitali ya KCMC kwa ajili ya taratibu nyingine.”

Ametoa wito kwa jamii kufanya kazi kwa bidii kujipatia kipato halali na kuacha imani za kishirikina za kutafuta utajiri au mafanikio kwa njia za mkato.

“Kutafuta utajiri au mafanikio kwa njia za mkato ni jambo ambalo halifai katika jamii na litaturudisha nyuma. Kama mtu anataka kupata utajiri afanye kazi kwa bidi, kwani haileti taswira nzuri kwamba leo tumekatisha uhai wa mtoto huyu kwa kuamini kupata utajiri,” amesema na kuongeza:

“Lakini niendelee kuisihi jamii, ulinzi wa mtoto ni jukumu letu wote na tusiwaache watoto katika maeneo bila uangalizi, kwani dunia imebadilika na watu wamekuwa na roho za tofauti.”

Mary Kiria, dada wa Bahati ambaye ni mtuhumiwa amesema siku ya tukio walikuwa nyumbani pamoja na mtuhumiwa na mtoto huyo wa jirani (marehemu).

Amesema: “Nilipokwenda kwa jirani kuchukua pilipili nilimuacha mtoto huyo (marehemu) akicheza na mwanangu mdogo huku akila chakula. Nikiwa njiani nilisikia mtoto akilia nilidhani amejichoma na chakula. Niliporudi nikamkuta mdogo wangu akitupa kitu shambani, nikamuita kumuuliza lakini alikimbia hakugeuka. Nilipiga kelele, ndipo watu walipokuja na mwili wa mtoto ukaonekana shambani.”

Mama wa mtoto huyo, Lucy Chuwa amesema: “Jana (Agosti 15) nilikuwa eneo la biashara yangu na nilikuwa na mtoto wangu Ivan, muda wa saa nane akaniambia mama naomba niende kwa mtoto nikamwambia ngoja nikupeleke. Nikaenda nikampeleka nikamkuta huyo dada yuko na mtoto wake hapo nje akaniambia muache hana shida, nikaondoka nikarudi kwenye biaahara yangu.”

“Baada ya saa moja nikasikia kelele hapo kwa jirani nikasema ni nini? Nikafunga duka haraka nikakimbia huko nilipofika nikauliza kuna nini hapa, nikaambiwa huyu kijana ameua mtoto nilipokwenda kuangalia nikakuta ni mwanangu na ameshakufa,” amesema.

Ameiomba Serikali ichukie hatua kali dhidi ya tukio hilo kwa kuwa mwanaye ameuawa kikatili bila kuwa na hatia yoyote.

Innocent Chuwa, baba wa mtoto huyo ambaye wakati wa tukio alikuwa akifanya shughuli zake za bodaboda, amesema alipigiwa simu akaambiwa mwanaye amechinjwa.

“Nilikimbia nyumbani nikamkuta mwanangu anatokwa damu shingoni akiwa anakakamaa na kufariki. Polisi walifika wakiwa na mtuhumiwa akiwa amechafuka damu. Sina ugomvi naye, ila alikuja hapa siku tatu tu zilizopita baada ya kurejea kutoka Babati, Manyara,” amesema.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Manushi Ndoo, Peter Massawe amesema baada ya mtuhumiwa kukimbia, alifuatwa na madereva wa bodaboda ambao walimkamata na alinusuriwa na polisi kutoka mikono ya wananchi.