Musoma Vijijini yapokea Sh208 milioni mradi wa maji

Musoma. Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara imepokea zaidi ya Sh208 milioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitano vya kuchotea maji katika vijiji vinne, mradi ambao ukikamilika unatarajiwa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

Fedha hizo zimetolewa na Serikali ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa uchimbaji wa visima 900 vya maji unaotekelezwa nchi nzima.

Akizungumza leo Jumamosi Agosti 16, 2025 wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Meneja wa Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) Wilaya ya Musoma, Edward Sironga, alisema utekelezaji wa miradi hiyo ulianza Januari mwaka huu na unatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka.

Amevitaja vijiji vinavyonufaika kuwa ni Muhoji, Masinono, Kiriba na Bugwema, huku akieleza kuwa ujenzi katika kijiji cha Muhoji umefikia asilimia 75 na utawanufaisha zaidi ya wakazi 1,200 wa kijiji hicho na vijiji vya jirani.

“Mradi huu utapunguza muda mrefu ambao wananchi walikuwa wakitumia kutafuta maji katika vijiji jirani,” amesema Sironga.

Baadhi ya wakazi wa Muhoji wamesema kukamilika kwa mradi huo kutamaliza changamoto kubwa ya maji waliyokuwa wakiipata.

Eliud Nyaubwa alisema wanawake walilazimika kutembea zaidi ya kilomita 10 kufuata maji kwenye visima vya asili, huku wengine wakilazimika kutumia maji ya madimbwi yasiyo salama.

“Nyingine tulikuwa tunalazimika kutumia maji pamoja na mifugo hali iliyochangia magonjwa ya mlipuko kama kuhara,” amesema Lucia Munema.

Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ussi, amesema Serikali inalenga kuboresha huduma za kijamii ikiwemo maji vijijini, jambo lililosababisha kuanzishwa kwa Ruwasa ili kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama.

“Upatikanaji wa maji safi na salama mbali na kuondoa changamoto kwa wananchi pia utawapa muda wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo,” amesema.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, amesema Mwenge wa Uhuru katika wilaya hiyo unatarajia kuzindua na kukagua miradi minane yenye thamani ya zaidi ya Sh2.5 bilioni ikiwemo elimu, afya, ustawi wa jamii na maendeleo ya vijana.