Arusha. Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa kibali kwa waliokuwa wafanyakazi wa kampuni ya Tanzanite One Mining Limited na mrithi wake, Sky Group Associates Limited, kufungua maombi ya mapitio dhidi ya Serikali.
Maombi hayo yalifunguliwa na Jonathan Kiula, Leonard Mmbaga, Herman Kassenga, Elija Rumbe na wenzao 466 ambao walikuwa wafanyakazi wa kampuni hizo dhidi ya Serikali ya Tanzania.
Uamuzi huo umetolewa Agosti 13, 2025 na Jaji Dafina Ndumbaro wa Mahakama Kuu kanda ya Arusha na nakala yake kupatikana leo Agosti 16, katika tovuti ya Mahakama inayochapisha maamuzi, sheria na kanuni mtandaoni.
Wafanyakazi hao 470 waliomba kibali hicho ili kufungua maombi kupinga uhalali wa wajibu maombi ambao ni Wizara ya Madini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), kusitisha leseni za kampuni hizo na kusababisha wao kupoteza kazi.
Kulingana na maombi hayo namba 5784 ya 2025, Serikali ilizisitishia kampuni hizo leseni ya uchimbaji madini namba ML. 490/2013 katika kitalu C, Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara na kuliweka eneo hilo katika usimamizi wa Jeshi.
Wanapinga hatua hiyo ya Serikali kwani imewafanya iwawie vigumu kwao kutekeleza tuzo ya shauri la kazi, ambalo walishinda na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ikaagiza walipwe Sh2.5 bilioni za malimbikizo ya mishahara.
Pia, wanakusudia kupinga uhalali wa wajibu maombi, kutoa eneo hilo la kitalu C Mirerani kwa mwekezaji mpya na hivyo kuwawia vigumu kutekeleza tuzo hiyo kwa kuwa mali za aliyekuwa mwajiri wao zipo eneo hilo linalolindwa na Jeshi.
Mbali na maombi hayo, kupitia kibali hicho cha Mahakama, wanakusudia kufungua maombi kupinga kitendo cha Serikali kuunda “ubia wa ulaghai na Sky Group” kwa makusudi tu ili kuipa kampuni hiyo kitalu hicho na kuwanyima haki zao.
Akiwasilisha hoja kwa niaba ya waleta maombi, wakili Frank Makishe, alisema wateja wake wanapinga mlolongo wa uamuzi wa kiutawala wa wajibu maombi, uliosababisha wapoteze ajira na kuwa vigumu kwao kutekeleza tuzo ya CMA.
Walifungua shauri CMA na kushinda na kutakiwa kulipwa Sh2.52 bilioni za malimbikizo ya mishahara lakini kwa kuwa Serikali imekabidhi mgodi kwa mwekezaji mpya, jitihada zao za kutekeleza tuzo hiyo zimeshindikana.
Wakili huyo alifafanua kuwa, awali waombaji walikuwa wameajiriwa na kampuni ya Tanzanite One na waliendelea kufanya kazi na mrithi wake ambaye ni Sky Group Associates Limited, ambayo iliingia ubia na Shirika la Madini la Taifa (Stamico).
Hata hivyo, wakili huyo alieleza kuwa baadaye iligundulika kuwa Sky Group Associates Limited ilikuwa haina usajili kutoka Wakala wa Usajili ya Leseni (Brela) na licha ya kufahamu hayo, Stamico iliingia ubia na kampuni hiyo.
Alisema baadaye Serikali ilisitisha leseni ya uchimbaji madini kwa sababu ya uharamu wa ubia, lakini bila kuzingatia masilahi ya ajira ya waombaji.
Kusitishwa huko kwa leseni pamoja na uwepo wa Jeshi katika kitalu hicho na uhai wa mwajiri kutokuwepo eneo hilo, umesababisha wajibu maombi washindwe kusukuma haki zao za kisheria, ikiwamo kulipwa Sh2.52 bilioni za mishahara.
Kwa mujibu wa wakili huyo, waleta maombi wamefanya jitihada mbalimbali za kukutana na kujadili na wajibu maombi bila mafanikio na badala yake wamekuwa wakipewa ahadi zisizotekelezeka na kutoa matamko ya kisiasa.
Alidai kuwa uwepo wa jeshi katika eneo hilo ambao wajibu maombi wanadai ni kwa ajili ya usalama, haujaweza kudhibiti shughuli haramu za uchimbaji madini kama ilivyoonyeshwa katika taarifa ya CAG kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Wajibu maombi kupitia kwa wakili wa Serikali, Zamaradi Nyamuryekung’e , walisema waombaji wameshindwa kufikia kigezo cha kisheria kinachohitajika ili kupewa kibali cha marejeo, kwa kuwa hawajaonyesha kesi inayobishaniwa, ukiukaji wowote wa sheria, wala masilahi ya kutosha inayoidhinisha uingiliaji kati wa Mahakama.
Pamoja na kutambua kuwa kibali ni takwa la kisheria la kuwezesha kufungua maombi ya mapitio ya Mahakama, wakili huyo anasisitiza kuwa kibali hicho kinapaswa kutolewa baada ya Mahakama kujiridhisha kuna kesi yenye mashiko.
Wakili huyo alieleza kusitishwa kwa leseni namba ML. 490/2013 ilikuwa ni halali kisheria kulingana na taratibu za kisheria, ikiwamo suala la ajira ya waombaji na kuwa hakuna haki ya msingi iliyovunjwa, wajibu maombi hawajatumia vibaya madaraka yao na uwepo wa Jeshi ni kwa sababu za kiusalama.
Kwa mujibu wa wakili huyo, waombaji walishindwa kubainisha sheria yoyote iliyovunjwa na mujibu maombi wa kwanza ambaye ni wizara ya madini na badala yake wameeleza tu kwa kirefu suala hilo bila kuonyesha kifungu kilichovunjwa.
Alieleza kuwa waombaji walipewa haki katika usikilizwaji wa shauri lao mbele ya CMA na waliondoa kwa hiyari yao kukazia tuzo hiyo na hivyo kufifisha msingi wa maombi yao na hivyo akataka maombi hayo yatupwe kwa kushindwa kukidhi viezo.
Uamuzi wa Jaji ulivyokuwa
Katika uamuzi wake, Jaji Ndumbaro alisema baada ya kuzingatia kwa umakini hoja za kisheria za pande mbili, Mahakama imebaini kuwa hakuna ubishi kuwa maombi yaliyoko mbele ya Mahakama yalifunguliwa ndani ya muda wa kisheria.
“Hoja ya kuamuliwa na Mahakama hii ni kama waombaji wameweza kuishawishi juu ya masilahi na hoja zinazoweza kusikilizwa na kutoa kibali cha kufungua maombi ya mapitio,” alisema Jaji Ndumbaro na kuongeza.
“Kutokana na mawasilisho ya pande mbili, Mahakama imeridhika kuwa waombaji wameonyesha kuwa haki na masilahi yao yameathiriwa na matendo ya kiutawala ya wajibu maombi katika shauri hili – Wizara ya Madini na AG).”
Jaji alisema kumbukumbu zinaonyesha waleta maombi walikuwa waajiriwa katika ubia baina ya mujibu maombi wa kwanza na kampuni ya Sky Group Associates Limited, ambayo waombaji wanadai ulikuwa hauna uhalali wa kisheria.
“Kufuatia kusitishwa kwa leseni ML.490/2013 na kuweka mgodi chini ya usimamizi wa jeshi, waombaji wameshindwa kukazia tuzo halali waliyoshinda CMA. Wajibu maombi hawajaleta sababu zozote za kisheria kueleza kwa nini wameshindwa kushughulikia tatizo la ajira ya waombaji au kusaidia utekelezaji wa tuzo,” alisema.
“Zaidi Mahakama inashawishika na swali lililoibuliwa na waombaji kuhusiana na uhalali wa kisheria wa kusitishwa kwa leseni, uwepo wa jeshi katika mgogoro wa kibiashara na kushindwa kwa wajibu maombi kutekeleza ahadi zao.
“Hiyo si hoja isiyo na mashiko, badala yake inaibua maswala mazito ambayo yanastahili kuchunguzwa na Mahakama. Mahakama inaona waombaji wameweza kutoa sababu za kutosha kuiwezesha kukubali maombi yao”
Jaji Ndumbaro alisema maombi hayo ya kupatiwa kibali cha kufungua maombi ya mapitio yanakubaliwa na wanapewa siku 14 kuyawasilisha mahakamani.