Nyamlani apeta tena TFF akiteuliwa Umakamu wa Rais

Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athuman Nyamlani amebaki katika nafasi yake baada ya kuteuliwa tena kuendelea na nafasi hiyo.

Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais anapatikana kwa kuteuliwa na Rais ambapo Karia ametumia fursa hiyo kumteua Nyamlani.

“Nimepokea uteuzi wa Rais kwa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwa mujibu wa Ibara ya 35 ya Katiba ambaye ni ndugu Athumani Nyamlani,” amesema Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Kiomoni Kibamba.

Kibamba pia amesema Karia ameteua wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji ya TFF kwa mujibu wa Katiba ambao ni Nyamlani, Evance Mgeusa, Debora Mkemwa na Azzan Salim.

Katika Uchaguzi wa TFF unaofanyika leo, wagombea sita wamefanikiwa kuwa washindi wa nafasi za ujumbe wa Kamati ya Utendaji.

Wajumbe hao ni Issa Bukuku, Salum Kulunge, Mohamed Aden, James Mhagama, Khalid Mohamed na Hosseah Lugano.