RC aliyekosa huduma hospitali, hatua zaanza kuchukuliwa kwa wahudumu

Moshi. Serikali imeshachukua hatua kwa wahudumu wa afya wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro, Mawenzi wanaodaiwa kutoa huduma zisizoridhisha kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro (RC), Nurdin Babu baada ya kumpeleka mwanaye hospitalini na kusubiri kwa saa tatu bila kuhudumiwa.

Agosti 12, 2025, wakati wa kikao cha tathmini ya hali ya lishe kwa mwaka 2024/2025, RC Babu alieleza kusikitishwa na namna hospitali hiyo inavyotoa huduma, akisema alikwenda akiwa amevalia kanzu na kofia kama mwananchi wa kawaida na wahudumu hawakumtambua.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Agosti 16, 2025, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro (RAS), Yusuf Nzowa amesema ufuatiliaji wa tukio hilo tayari umefanyika na uongozi wa hospitali umewasilisha maelezo kwa maandishi.

“Tumefanya ufuatiliaji na kumuelekeza Mganga Mfawidhi wa Mawenzi kutuletea taarifa ya kilichotokea Agosti 9 saa tatu usiku. Hadi sasa, taarifa hizo zimewasilishwa na wahudumu waliokuwa zamu nao wameandika maelezo yao. Vikao vya kiutendaji vinaendelea na yeyote atakayebainika kufanya uzembe atachukuliwa hatua za kinidhamu,” amesema Nzowa.

“Mpaka sasa hivi Mganga Mfawidhi wa hospitali ameleta taarifa yake ya kueleza ni nini kilichotokea siku hiyo Agosti 9, na wale wahudumu wa afya waliokuwa zamu wamewasilisha taarifa yao ya maandishi kwa uongozi wa hospitali.”

Aidha, ametoa wito kwa wahudumu wa afya kufanya kazi kwa weledi na kwa kujituma wakijua wanawatumikia wananchi Watanzania.

“Wito wangu kwa hospitali ile, kwasababu ni hospitali inayotegemewa na watu wengi, kuwataka watumishi na watendaji wote katika hospitali wafanye kazi zao kwa weledi, kwa kujituma wakijua wanawatumikia wananchi ambao ni walipa kodi wa nchi hii,” amesema Nzowa

“Lazima kila mtumishi iwe ni dereva, mhudumu, muuguzi, daktari kwenye akili yake ajue yupo pale kuwahudumia wananchi ndio maana serikali hii inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka fedha nyingi katika sekta ya afya.”

Nzowa amebainisha hospitali hiyo imenufaika kwa kiasi kikubwa na uwekezaji wa vifaa tiba na watumishi, hivyo hakuna sababu ya kuwepo malalamiko ya huduma duni.

Amesisitiza uongozi wa hospitali unapaswa kufuatilia kwa karibu utendaji wa kila mtumishi na kuchukua hatua stahiki kwa watakaoonekana kutotekeleza wajibu wao ipasavyo.

“Watumishi wa afya wanapaswa kufanya kazi zao kwa weledi na kujituma wakiamini wanawahudumia Watanzania, hivyo kila mtu atoe huduma kwa kiwango kinachoridhisha, anapokuja mgonjwa hospitalini ahudumiwe kwa wakati sahihi na kwa haraka kwa kiwango ambacho hakitaleta malalamiko wala lawama,” amesema Nzowa.

Amesema:”Watumishi wote wa hospitali yetu ya Mawenzi na hata uongozi tumeusisitiza hivyo ufuatilie kwa karibu utendaji wa watumishi wote na wale ambapo kunaonekana kuna watumishi wachache ambao hawatimizi vyema majukumu yao basi hatua stahiki za kinidhamu za kiutumishi zichukuliwe.”