Shinyanga. Wakati shughuli za uokoaji zikiendelea kwenye mgodi wa Chapakazi wilayani Shinyanga ili kuwapata watu 18 walionasa ardhini, Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa ameagiza kuchunguzwa migodi yote nchini ili kuepuka majanga.
Ametoa agizo hilo leo Agosti 16, 2025 alipozungumza na wananchi eneo la ajali mgodini katika Kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge, wilayani Shinyanga.
“Natoa agizo kwa wakaguzi wa migodi, yote ichunguzwe ili kuepuka ajali zinazotokea na kusababisha kupoteza uhai wa watu, pia tusikate tamaa, kukata tamaa ni dhambi. Bado Serikali ina matumaini ya kutoa watu wetu wakiwa hai, tuendelee kuombeana,” amesema.
Ajali hiyo ilitokea Agosti 11, 2025 wakati eneo la mduara wa mgodi likikarabatiwa na kusababisha watu 25 kufukiwa.
Mkaguzi Mkuu wa kikundi cha Wachapakazi Gold Mine, Fikiri Mnwagi ambao ni wamiliki wa mgodi huo, alisema maduara matatu yalititia wakati wa ukarabati.
Agosti 12, watatu waliokolowa wakiwa hai na wawili wamesharuhusiwa kutoka hospitali, mmoja alipewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza kwa matibabu zaidi.

Agosti 13, mtu mmoja aliokolewa akiwa na majeraha na alifariki dunia akipatiwa matibabu hospitalini. Agosti 15, mwili wa mtu mmoja uliopolewa na kutambuliwa kuwa wa Magunda Ng’ondi (28).
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro amesema watu wawili wamegundulika walipo ardhini na juhudi za kutoa mawe na vizuizi vingine zinaendelea ili kuwatoa.
“Kwa kutumia mashine za utambuzi, waokoaji wamefanikiwa kugundua watu wawili maeneo walipo ardhini, juhudi za kuwatoa zinaendelea na kuwatafuta wengine ambao bado hatujafanikiwa kuwapata,” amesema Mtatiro na kuongeza:
“Ofisi ya mtendaji wa kijiji iwekwe hapa kwa muda, itatumika kusaili wageni waliotoka nje ya kijiji kwa ajili ya kusubiria ndugu zao waliofukiwa, ili waweze kupewa mahitaji muhimu ya kibinadamu.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Daniel Sillo, amepongeza juhudi za uokoaji zinazoendelea, kwa ushirikiano wa jamii na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.
“Nitoe pongezi kwa viongozi wa eneo hili ambao bado wanaendelea kusimamia zoezi hili kwa kushirikiana na wananchi na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji. Pia, Msalaba Mwekundu kwa juhudi hizi zilizofanyika na zinazoendelea kufanyika” amesema.
Mtatiro alisema jana Julai 15 kuwa yapo matumaini ya kuwapata walionasa ardhini wakiwa hai kwa kuwa hewa inaingia, akirejea tukio la Nyangalata Novemba 2015, mkoani Shinyanga, ambako wachimbani waliokolewa baada ya siku 41.
Pamoja na juhudi zinazoendelea baadhi ya ndugu wa waliofukiwa mgodini wameiomba Serikali iziongeze, huku wakiwa wamejiandaa kwa matokeo yoyote.