Arusha. Serikali imesema itaendelea kuhakikisha waandishi wa habari wanafanya kazi katika mazingira salama, bila vitisho wala bugudha wakati wote wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025.
Hayo yamesemwa leo Agosti 16, 2025 na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Habari Maelezo, Rodney Thadeus wakati wa mafunzo ya waandishi wa habari na watangazaji kuelekea uchaguzi Mkuu wa 2025, yanayofanyika katika ukumbi wa AICC Arusha.
Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) yamejumuisha waandishi wa habari kutoka mikoa minne ya Kanda ya Kaskazini, Tanga, Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
“Ndiyo maana mkutano huu umehusisha vyombo vya ulinzi na usalama ili kwa pamoja tuhakikishe waandishi wa habari wanafanya kazi katika mazingira salama bila vitisho, wala bugudha,” amesema
Amesema “Wakati taifa linajiandaa kuingia kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu, ni dhahiri kuwa sekta ya habari imebeba dhamana kubwa ya kuhakikisha kuwa mchakato huu unafanyika kwa amani, usawa na kwa uelewa wa kutosha kwa wananchi,” amesema Thadeus.
Mbuya, amesema kipindi hiki ni kipindi ambacho jamii ina matarajio makubwa ya kupata taarifa sahihi kwa wakati na zisizo na upendeleo wowote katika vyombo vya habari.
“Hii inatufanya tuone umuhimu wa kukutana na kujadiliana pamoja, kuweka misingi madhubuti ya ushirikiano kati ya serikali, vyombo vya habari na waandishi wa habari, asasi za kiraia, Taasisi za usalama, Taasisi huru kama INEC,”
Amesema, “Ili kuhakikisha tunalinda amani, kuhimiza usawa, fursa kwa vyama vyote vya siasa na kuruhusu wananchi kupata taarifa za msingi zitakazowezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuchagua viongozi wao ifikapo Oktoba mwaka huu.”
Pamoja na mambo mengine, amesema maendeleo ya teknolojia na mitandao ya kijamii imekuwa na changamoto mpya ikiwemo upotoshaji wa taarifa, lugha za chuki na habari zisizo na uthibitisho.
“Katika mazingira ya leo ya maendeleo ya teknolojia na mitandao ya kijamii tunakabiliwa na changamoto mpya ikiwemo ya upotoshaji wa taarifa , lugha za chuki, habari zisizo na uthibitisho,” amesema Thadeus.
Awali akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa wilaya ya Longido, Salum Kalli, aliwataka waandishi wa habari wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini kujiepusha na habari za uzushi, upendeleo, potofu na uchochezi.
Amesema ni muhimu kutambua kuwa kuzingatia maadili ni takwa la kisheria hivyo wana wajibu wa kuhakikisha wanatumia kalamu zao vizuri ili kutoleta taharuki kwa jamii.
Mkuu huyo amesema kuwa sekta ya habari ina wajibu wa kuhakikisha inatimiza wajibu wake kwa kuzingatia sheria ikiwemo kuibua na kufuatilia ukiukwaji wa sheria, kuhamasisha makundi maalum kushiriki uchaguzi mkuu.
“Waandishi wa habari mnapaswa kupambana na taarifa potofu, mjiepushe na habari za uzushi, upendeleo na uchochezi, mjiepushe na rushwa na mna wajibu wa kutambua maadili ya habari si hiari ni wajibu,” amesema.
“Mafunzo haya yanatolewa kwa wakati muhimu tunapoelekea kwenye uchaguzi, kalamu ya waandishi wa habari ikitumiwa vibaya inaweza kuleta taharuki na madhara kwenye jamii, Tanzania itakuwa tulivu na yenye amani mkitumia kalamu zenu vizuri na Serikali itaendelea kulinda vyombo vya habari ,”ameongeza.
Akitoa mada kuhusu mwongozo wa waandishi wa habari katika uandishi wa habari za uchaguzi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Egbert Mkoko amesema Idara ya Habari Maelezo kwa kushirikiana na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC), imeandaa mwongozo huo.
Amesema lengo la mwongozo ni kutoa mwelekeo wa kitaaluma na kimaadili.
“Mwongozo umelenga pia kuhakikisha kunakuwa na haki, usawa, uwazi na weledi katika utoaji wa taarifa kwa umma ili kukuza demokrasia nchini,” amesema Dk Mkoko.
“Kuchukua tahadhari dhidi ya matumizi mabaya ya majukwaa ya habari na kuhakikisha vyama na wagombea wake wanapewa fursa katika kufanikisha ujumbe na sera zao kwa wananchi na kutoa dira kwa vyombo vya habari ili visaidie kulinda amani na utulivu wa taifa kwa kuepuka kuchapisha maudhui yenye viashiria vyenye uchochezi au upotoshaji ,”
Meneja wa Huduma za Utangazaji, kutoka TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka amesema kanuni za utangazaji wa uchaguzi kwa vyama vya siasa za mwaka 2020,zinaelekeza namna uchaguzi unatakiwa kuripotiwa.
Amesema kanuni ya 4(a) (b), inaelekeza utangazaji wa habari katika uchaguzi wa vyama vya siasa, unaripotiwa na kuwasilishwa na kuwasilishwa bila upendeleo na kwa uadilifu bila kuonyesha mtazamo binafsi wa mtazamaji.
Amesema kifungu hicho kinaeleza suala lililopo katika mdahalo wa umma, unatendewa haki kwa maslahi ya wote na kwamba suala linalotangazwa linawasilishwa bila upendeleo.