Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeipongeza Jamhuri ya Watu wa China kwa kusimama imara katika kulinda amani na haki za watu wake dhidi ya uvamizi kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Pongezi hizo zimetokewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana wakati wa maonyesho ya picha za kihistoria yenye lengo la kukumbuka historia, kuenzi mashujaa waliopoteza maisha, kujenga mustakabali bora.
Mwaka huu, China inaadhimisha miaka 80 ya ushindi wa vita vya ukombozi wa watu wa China dhidi ya uvamizi wa Wajapani, vita dhidi ya ufashisti na kurejeshwa kwa kisiwa cha Taiwan chini ya umiliki wa China.
Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika usiku wa Agosti 15, 2025, Dk Pindi amesema maonyesho hayo yanakumbusha yanaufanya umma kukumbuka jinsi mashujaa walivyojitoa kwa kuthamini amani inafurahiwa leo.
“Ushirikiano na maelewano kati ya Mwalimu Julius Nyerere na ndugu yake wa China, Mwenyekiti Mao Ze Dong ulichochea amani kwa sababu walihubiri amani na ushirikiano. Hata leo Rais Samia Suluhu Hassan ameweka msisitizo kwenye suala la amani, ushirikiano na maridhiano,” amesema Dk Pindi.
Ameongeza miaka ya 1970, China na Tanzania zilianza kubadilishana tamaduni ikiwa ni mwendelezo wa ushirikiano uliokuwepo katika maeneo mengine kama vile miundombinu, elimu, afya na kilimo.
“Naipongeza Jamhuri ya Watu wa China kwa kuchangia katika amani ya dunia. Nimefurahi kusikia balozi (wa China nchini Tanzania) akisema China imekuwa ikichangia Umoja wa Mataifa (UN) tangu miaka ya 1940 baada ya vita vya pili vya dunia,” amesema.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian amesema Agosti 15, 1945, Japan ilitangaza kujisalimisha bila masharti tukio kubwa lililowakilisha ushindi wa vita ya ukombozi wa watu wa China dhidi ya uvamizi wa Wajapani na vita vya dunia dhidi ya Ufasisti.
“Vita vya dunia dhidi ya ufasisti vilikuwa na ukubwa usio na kifani katika historia ya binadamu, vikihusisha zaidi ya nchi na maeneo 80 na watu wapatao bilioni 2. Nchi na watu waliopenda amani na haki walinyanyuka kupigana na kujenga umoja wa dunia nzima dhidi ya ufashisti,” amesema.
Amesema kupitia miaka 14 ya mapambano magumu na yenye kumwaga damu, na kwa sadaka kubwa ya zaidi ya askari na raia wa China milioni 35 waliopoteza maisha au kujeruhiwa, wananchi wa China walisimama imara katika uwanja mkuu wa vita vya Mashariki mwa dunia dhidi ya ufasisti vita ambavyo vilianza mapema na kudumu muda mrefu zaidi na hatimaye wakapata ushindi mkubwa dhidi ya uvamizi wa Kijapani.
“Wachina hawakulinda tu uhuru wa taifa lao na umoja wa mipaka yao, bali pia walitoa ushirikiano na msaada muhimu kwa vita kuu ya uzalendo ya umoja wa kisovieti, vita ya Pasifiki, na mapambano ya kupinga ufasisti Afrika Kaskazini, Bahari ya Mediterania na Kusini-Mashariki mwa Asia. Haya yote yalikuwa mchango mkubwa usioweza kufutika wala kubadilishwa katika ushindi wa mwisho wa vita vya dunia dhidi ya ufasisti,” amesema.
Ameongeza kuwa ushindi huo mkubwa ulikuwa matokeo ya mshikamano wa pamoja wa wananchi wote wa China pamoja na washirika wake wa kupinga ufashisti na watu wa dunia nzima. Amesema utabaki daima katika historia ya jitihada za kutafuta haki kwa ajili ya ubinadamu wote.
Awali, akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dk Noel Lwoga amesema maonyesho hayo ni sehemu muhimu katika ushirikiano wa Tanzania na China na wanaahidi kuendelea kushirikiano katika kuhifadhi kumbukumbu muhimu za ushirikiano baina yao.
“Makumbusho ya Taifa tumekuwa tukishirikiana na balozi mbalimbali zilizopo hapa nchini, tunafurahi kushirikiana na China katika maonyesho haya muhimu kwani yanatukumbusha historia ya China, jinsi ilivyopambana kulinda amani na mustakabali wake,” amesema Dk Lwoga.