Kilwa. Serikali inategemea kutumia kiasi cha Sh114bilioni kwaajili ya ujenzi wa madaraja 11 na maboksi 18 ambayo hadi sasa ujenzi wake umefikia zaidi ya asilimia 75 .
Akizungumza leo Jumamosi Agosti 16,2925 baada ya kutembelea na kufanya ukaguzi katika maeneo ambayo mvua za El-nino ziliharibu miundombinu katika mikoa ya kusini, Mtendaji mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta amemtaka Meneja wa Tanroads mkoa wa Lindi kuongeza Nguvu za kusimamia wakandarasi.
Besta ameendelea kufafanua kuwa ujenzi uendelee kwa kasi ili wananchi wa mikoa ya kusini waondokane na adha ya za usafiri kwani barabara ya kusini imekuwa ni kichocheo cha uchumi.
“Usimamizi ni mzuri lakini nimuombe Meneja wa Tanroads mkoa kuongeza usimamizi kwa wakandarasi ili kumaliza kazi wakati na wananchi waendelee kutumia barabara hiyo bila shida yoyote,” amesema Mhandisi Besta.

Naye Meneja wa Tanroads mkoa wa Lindi Mhandisi Emily Zengo amesema kuwa madaraja yote yanayojengwa yamefikia asilimia 75,na amesema kuwa vyuma vya kumalizia ujenzi huo vimeagizwa kutoka nchini China na wakati wowote vitafika ili kuweza kumalizia ujenzi wa madaraja.
Mhandisi Zengo amewatoa hofu wasafirishaji kuwa madaraja hayo yatakamilika kwa wakati na wananchi wataendelea na shughuli zao kama kawaida bila kupata adha yoyote.
“Madaraja haya yapo 11, maboksi karavati yapo 18,Serikali ilitenga kiasi cha Sh.114bilioni kwaajili ya ujenzi ya madaraja na maboksi karavati, niwatoe wasiwasi wananchi wa mikoa ya kusini na wasafirishaji kuwa madaraja hayo yatakamilika kwa wakati,” amesema Mhandisi Zengo.
Mhandisi Salumu Utali kutoka kamapuni ya ujenzi ya Makapo ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwaajili ya ujenzi wa madaraja kwani barabara hiyo ya kusini ilikuwa imekatika madaraja mengi na kushindwa kufanya safari kuelekea mikoa ya Dar es Salaam na mikoa ya kusini.

“Kikubwa sisi tunashukuru serikali kwa kutoa fedha kwaajili ya ujenzi wa madaraja katika barabara ya kusini na sisi kama makapu tupo hapa tunajenga Daraja la Mikereng’ende na ujenzi wake umefikia asilimia 75,imani yangu kubwa tutamaliza kwa wakati ujenzi wa daraja hili.” amesema Utali.
Hadija Seifu mkazi wa Kilwa ameishukuru Serikali kwa jitihada kubwa waliyoifanya kwa kutoa fedha kwaajili ya ujenzi wa madaraja yaliyoharibiwa na mvua za kimbunga Hidaya.
“Sisi wananchi wa kusini tunaishukuru serikali kwa jitihada kubwa walizofanya kwa kutoa fedha kwaajili ya ujenzi wa madaraja na ni fursa pekee kwetu watu wa Kilwa kufanya biashara kwa wageni ambao wamekuja kujenga haya madaraja,” amesema Seifu.