JANA, mabingwa wa Afrika Kusini, Mamelodi Sundowns walimuaga nyota wao baada ya kuwatumikia kwa miaka minne ambapo Masandawana walielezea kufurahia kipindi alichodumu ndani ya chama lao na kumtakia kila la heri katika safari yake ya soka.
Huyu si mwingine, bali ni Neo Maema, fundi anayeiongoza Afrika Kusini katika michuano ya CHAN 2024 inayoendelea Tanzania, Kenya na Uganda ambapo tayari ameshaifungia nchi yake bao moja matata jambo ambalo linabaki kuwa histori kwake na nchi yake katika soka.
Lakini, kilicho wazi ni kwamba hakuna siri tena kwamba Simba itamtambulisha tu kiungo huyo mshambuliaji baada ya mabosi wa Msimbazi kumpandia ndege ili kuwahi dirisha la usajili la CAF.
Usajili wa nyota huyo Msauzi ulikuwa haujakamilika kama ilivyokuwa inaripotiwa, lakini kuna akili moja ya maana ambayo mabosi wa Simba walifanya kuamua kutuma mtu Afrika Kusini ili kuweka mambo sawa kabla ya kufungwa kwa dirisha hilo la usajili.
Kama ulikuwa hufahamu ni kwamba jana Ijumaa Agosti 15, 2025, ilikuwa mwisho wa klabu inayotaka kumfanyia uhamisho mchezaji kufanya hivyo.
Na hapo ndipo Simba katika kuhakikisha inaiwahi huduma ya Maema kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, ikamsafirisha Ofisa Mtendaji Mkuu, Zubeda Sakuru hadi Afrika Kusini.
Dili hilo la Maema lilikamilika juzi usiku baada ya vikao vya siku mbili kati ya Sakuru na mabosi wa Mamelodi Sundowns ambao mapema jana asubuhi Masandawana walimuaga rasmi fundi huyo wa boli anayemiliki bao moja katika fainali za CHAN zinazoendea Tanzania, Kenya na Uganda.
Maema aliagwa na wababe hao wa Sauzi baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa mafanikio kwa miaka minne akiwa tayari kujiunga na Simba kwa msimu ujao wa mashindano.
Mchezaji huyo ndani ya Sundowns ameshinda mataji saba yakiwemo manne ya Ligi Kuu Afrika Kusini, moja Kombe la Nedbank na jingine la MTN8 mbali na ubingwa wa African Football League (AFL).
Katika miaka minne kiungo huyo akiwa Mamelodi amecheza mechi 120 akifunga mabao 13 na kutengeneza asisti 14.
Kiungo huyo atajiunga na Simba mara baada ya kumalizika kwa fainali za CHAN akiwa tayari ameshafunga bao moja katika kikosi cha Afrika Kusini ambacho ndicho nahodha wake.
Maema ni chaguo la kocha Fadlu Davids ambaye amependekeza usajili wake ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi msimu ujao.