TIMU ya taifa ‘Taifa Stars’ imelazimishwa suluhu na Afrika ya Kati kwenye mechi ya mwisho ya kundi B iliyopigwa katika Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Stars ilishafuzu mapema robo fainali baada ya kuichapa Madagascar mabao 2-1 siku chache zilizopita kwa mabao yaliyofungwa na Clement Mzize ambaye leo hakuwa sehemu ya mchezo.
Stars ambayo iliingia kwenye mechi hiyo ikiwa na mabadiliko ya wachezaji watano waliocheza mechi tatu lakini hii walianzia benchi wakiwapa nafasi nyota wengine.
Wachezaji hao ni Idd Seleman ‘Nado’ aliyeingia kipindi cha pili akichukua nafasi ya Shekhan Khamis, Nassor Saadun aliyechukua nafasi ya Ibrahim Hamad ‘Hilika’ na Lusajo Mwaikenda aliyemaliza dakika 90 eneo ambalo Shomari Kapombe alianza mechi za awali.
Ahmed Pipino alianza akichukua nafasi ya Mudathir Yahya ambaye hakuwepo hata benchi na Pascal Msindo kwenye eneo la Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Licha ya juhudi za Stars kupambana kupata bao kupitia mipira mirefu na kona, lakini Afrika ya Kati waliziba mianya hiyo.
Sare hiyo inaifanya Stars isalie kileleni mwa msimamo wa kundi B ikiwa na pointi 10 na Madagascar iliyoshinda 2-1 dhidi ya Burkina Faso huko Zanzibar inaungana na Tanzania kwenda robo fainali.
Kikosi cha Stars: Yacoub Suleiman, Ibrahim Hamad, Dickson Job, Feisal Salum, Ahmed Pipino, Abdul Hamis Suleiman, Pascal Msindo, Lusajo Mwaikenda, Ibrahim Hamad ‘Hilika’, Yusup Kagoma.
Kikosi cha Afrika ya Kati: Mauril Abimala, Cyrille Judicael, Flory Jean, Cherubin Merlus, Fourdeau Miambaye, Zoumara Ange Heritier Namsona, Benjamin Leance, Kogbeto Dimitri, Donald Guesset.