Taifa Stars kazi ile ile, muda uleule CHAN

TAIFA Stars imeshafuzu robo fainali za michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024, lakini kocha mkuu Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesisitiza kazi haijaisha na kwamba leo wanakamilisha ratiba, huku dhamira ni kupata ushindi ili kuboresha rekodi waliyoiweka.

Stars itashuka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 2:00 usiku muda ambao timu hiyo imekuwa ikicheza mechi zake za Kundi B ili kuvaana na Afrika ya Kati ambayo imeshaaga mashindano kutokana na kupoteza mechi zote tatu za awali za kundi.

Mechi hiyo itaenda sambamba na ile itakayopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar inayozikutanisha Madagascar na Burkina Faso za kundi B zinazopambana kuing’oa Mauritania yenye pointi saba iliyomaliza mechi zake.

Kwa mechi ya Dar es Salaam itakuwa ya nne kwa timu hizo kukutana tangu 2011.

Awali zilishacheza mara tatu zikiwamo mbili katika makundi ya kuwania fainali za Afcon na kila moja ilishinda nyumbani 2-1 na ile ya mwisho ilikuwa ya kirafiki  Machi 23, 2022 na Tanzania kushinda mabao 3-1.

Licha ya Tanzania imeshafuzu robo fainali na sasa inasubiri mechi za Kundi A zitakazopigwa kesho Jumapili kujua timu ipi itakayokutana nayo katika hatua inayofuata kutokana na ukweli vinara na wenyeji wa kundi hili, Kenya, Morocco na DR Congo kila moja ina nafasi ya kumaliza nafasi ya pili.

Kwa mujibu wa ratiba ilivyo ni kwamba mshindi wa kwanza wa Kundi A atacheza na mshindi wa pili wa kundi B na inayomaliza nafasi ya pili kutoka Kundi A ataumana na kinara wa Kundi A ambayo ni Tanzania kwani imekusanya pointi tisa kupitia mechi tatu na haziwezi kufikiwa na timu nyingine.

Kocha Morocco aliyeweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza mzawa kuiongoza Stars kucheza mechi tatu mfululizo za makundi ya michuano ya CAF bila kupoteza, lakini kuipeleka timu robo fainali alisema anajua mechi haitakuwa rahisi licha ya kwamba Stars imeshafuzu na Afrika ya Kati kuaga.

“Hakuna mechi rahisi, tutashuka kama tunaisaka nafasi ya kufuzu kwa vile kusudio ni kuendelea kuwapa burudani mashabiki wa Stars kabla ya kuanza kazi kwa mechi ya hatua ijayo, mashabiki waje wapate raha, kwa vile tutashuka kupambana kwani Afrika ya Kati haitakuja kinyonge,” alisema Morocco na kuongeza akisisitiza kikosi kipo tayari kwa mchezo wa leo ili kupata ushindi wa nne.

Stars itaendelea kuwategemea nyota walioifikisha hapo ilipo akiwamo kipa Yakoub Suleiman aliyeruhusu bao moja tu katika mechi tatu.

Hata hivyo, huenda kocha Morocco akafanya mabadiliko kidogo kwa baadhi ya wachezaji katika mechi hiyo ili kutunza nguvu kwa ajili ya pambano lijalo la robo fainali litakalopigwa Agosti 22, jijini Dar es Salaam kutokana na yenyewe kuongoza Kundi B.

Kwa mechi ya visiwani Zanzibar inayopigwa pia kuanzia saa 2:00 usiku, makocha wa timu zote wametambiana, huku Madagascar wakipiga hesabu kali za kupata ushindi mnono ili kuipiku Mauritania wenye kumiliki pointi saba. Madagascar ina uwezo wa kufikisha pointi saba pia, hivyo uwiano wa mabao baina yao na wenzao ndio itaamua wa kuambatana na Tanzania kucheza robo fainali, wakati Burkina Faso anatafuta kumaliza michuano hiyo kwa heshima kwani ina pointi tatu.

Mauritania imefunga mabao mawili na kufungwa moja, wakati Madagascar imefunga mabao matatu na kufungwa mawili, kitu kinachoipa jeuri ya kuibana Burkina Faso ili imalize nafasi ya pili, japo inapaswa iwe makini na wapinzani wao wanaoonekana wana safu kali ya ushambuliaji, japo ina udhaifu wa kuruhusu mabao kwani katika mechi tatu zilizopita za kundi hilo imefunga manne na kufungwa matano.