TMDA yatahadharisha uwepo wa Dettol bandia, yatoa mbinu kuzibaini

Dar es Salaam. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetahadharisha uwepo wa Dettol za maji bandia zilizokutwa zikitengenezwa kinyume cha sheria katika nyumba ya kulala wageni iliyopo Mtaa wa Namanga, Kahama mjini mkoani Shinyanga.

Raia wawili wa kigeni kutoka nchi jirani, wanashikiliwa baada ya kuhusika na uzalishaji wa Dettol hizo bandia zenye ujazo wa 50ml, 125ml, 250ml, 500ml na Lita1 na kubandikwa lebo kuonyesha kwamba ni Dettol zilizo halisi.

Taarifa iliyotolewa leo Jumamosi, Agosti 16, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo imeeleza kupitia mifumo ya ukaguzi na ufuatiliaji wa bidhaa katika soko iliyowekwa wamebaini uwepo katika soko wa Dettol hizo za maji.

Amesema utengenezaji wa Dettol hizo bandia umebainika kufuatia taarifa za kiintelijensia zilizokusanywa na TMDA na kisha ukaguzi uliofanywa kwa pamoja na Jeshi la Polisi katika nyumba moja ya kulala wageni inayoitwa New Kishimbe Lodge iliyopo Kahama mjini.

“Katika nyumba hiyo kulikutwa malighafi mbalimbali zikiwemo vifaa, kemikali na vyombo kama vile chupa tupu za Dettol, lebo, rangi, madumu makubwa na vimiminika katika chumba kimojawapo walichokuwa wanaishi raia wawili kutoka nchi jirani ambao wanatuhumiwa kushiriki katika uhalifu huo,” amesema Fimbo.

Amesema watuhumiwa waliohusika na uhalifu huo wamefikishwa katika vyombo vya usalama na tararibu za kuwafikisha Mahakamani zinaendelea ili kuweza kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.

Fimbo ametoa maelezo namna ya kuitambua Dettol hiyo bandia, kwa kuangalia namba za matoleo.

Amesema baadhi ya Dettol bandia zimegushiwa namba za matoleo (batch numbers) na kuandikwa P08 08 24R25 na P08 02 24R25.

“Kifuniko cha chupa hakina kifungo (lock) kinachounganisha na bangili ya chini. Hivyo kinafunguka kirahisi. Pia lebo zinafanana na halisi lakini za Dettol bandia zinabanduka kirahisi sana pia kuna utofauti mkubwa kwenye muonekano wa lebo bandia,” amesema Fimbo.

Amesema kutokana na kubainika kwa Dettol hizo bandia, TMDA inapenda kuwashauri wananchi wote wanaotumia Dettol za maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kuuwa vijidudu kuangalia kwa makini lebo zake na endapo watatilia mashaka watoe taarifa kwenye Ofisi za TMDA zilizo karibu au kituo cha Polisi.

Aidha, amesema wafanyabiashara wanaojihusisha na ununuzi wa bidhaa hizo, wanaelekezwa kununua Dettol kutoka katika vyanzo halisi na kupewa risiti kwa manunuzi waliyofanya.

“TMDA inatoa onyo kwa kampuni, kikundi, mitandao au mtu yeyote anayejihusisha na utengenezaji, usambazaji au uuzaji wa dawa ikiwemo vipukusi, vifaa tiba na vitendanishi duni na bandia kwani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” amesema.

Aidha, amebainisha kuwa TMDA inaendelea kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa TMDA au vituo vya Polisi wanapobaini uwepo wa ukiukwaji ya Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba Sura 219 ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa lengo la kulinda afya ya jamii.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara walioulizwa iwapo wanafahamu kuhusu uwepo wa bidhaa hizo, wamesema mara nyingi bidhaa hizo huuzwa katika maduka ya jumla ambayo hata hivyo baadhi ni ngumu kufahamu kama si halisi.

“Utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara na umma kwa ujumla unasaidia kujua kama bidhaa tunazonunua kwa ajili ya kupeleka kwa jamii ni halisi au vinginevyo,” amesema Juma Omary mfanyabiashara wa duka Tabata jijini Dar es Salaam.