Ubebaji huu hatari kwa mtoto chini ya miaka mitano

Dar es Salaam. Mazoea ya baadhi ya watu kuwabeba watoto wadogo chini ya miaka mitano kwa kuwashika mikono na kuwavuta juu, kuwaweka kichwani au shingoni na kisha kuwashusha kwa njia ileile, yanatajwa na wataalamu wa afya kuwa ya hatari kwa usalama wao.

Wapo pia wazazi na walezi wanaowaburuza watoto kwa kuwashika mkono wanapokataa kutembea, wakidhani ni njia ya kuwahimiza kutii.

Mbali ya hao, wapo wanaocheza na watoto kwa kuwazungusha wakiwa wamewashika mikono huku miguu ikiwa juu.

Vitendo hivi kwa mujibu wa wataalamu wa afya vinaweza kuathiri ukuaji wa mifupa, mishipa na viungo vya watoto ambavyo bado havijakomaa.

Kumbeba mtoto wa umri huo kwa kumuinua kwa kumshika mikono badala ya chini ya kwapa ni hatari kwa sababu unamuweka katika hatari ya kuhama kwa kiungo cha kiwiko. Hii ni hali inayotokea pale kiwiko kinapopata mvuto wa ghafla, kama vile mtoto kuinuliwa au kuvutwa kwa nguvu kwa mkono ulionyooshwa.

Kitalamu inaelezwa watoto wadogo wana mishipa ya viungio (ligaments) na mifupa midogo yenye tishu laini zaidi kuliko watu wazima. Hivyo, kumvuta mtoto kwa mikono kunaweza kusababisha mfupa mdogo wa mkono kutoka sehemu yake kwenye kiwiko.

Amina Ramadhan, mkazi wa jijini Dar es Salaam akizungumza na Mwananchi anasema aliwahi kupata changamoto ya aina hiyo alipomnyanyua mtoto wake wa miaka miwili, jambo lililosababisha alie usiku kucha kutokana na maumivu.

“Nilihisi mtoto wangu amevunjika mkono, kulipokucha nikakimbia hospitali, sikuwa na ujuzi wowote juu ya hali hiyo. “Tulipofika akasaidia na daktari na sasa anaendelea vizuri. Nakiri tatizo hili halijawahi kujirudia tena maana ushauri wa daktari aliotupatia naufanyia kazi,” amesema.

Akitoa ushuhuda katika ukurasa wa dondoo za afya wa Veriafya, Grace Kasiri anasema mtoto wake aliwahi kupitia hali hiyo kutokana na kuvutwa na jirani yake.

“Mtoto alilia saa tatu nikampeleka hospitali kutibiwa ingawa hivi sasa umekuwa kama ugonjwa, kwani ukikosea tu kumshika inakuwa shida,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi, Dk Daud Emmanuel kutoka Zanzibar anasema watoto wadogo hupata maumivu japokuwa mara nyingi mkono hauvimbi wala kuonekana wazi kama umevunjika.

“Hivyo mara nyingi wazazi wanashindwa kutambua kwa haraka tatizo au kutojua chanzo cha tatizo maana mtoto huwa hajaanguka au labda alikuwa anacheza tu na wazazi au ndugu wengine,” amesema.

Dk Fabian Maricha anasema hairuhusiwi kumnyanyua mtoto kwa kumshika mikono kwa sababu ya hatari iliyopo, kwani unaweza kutenganisha viunganishi vya misuli na mifupa ya mikono.

“Kumbuka mkono wako ni mzito kuliko uzito wa mkono wa mtoto kwa sababu hiyo mtoto anakuwa ni kama kanyanyua kitu kizito,” amesema.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, kuumizwa mara kwa mara kunaweza kusababisha kulegea kwa kiwiko au mtoto kupata maumivu ya kudumu.

Kwa mtoto aliyeumia inaelezwa atakuwa na maumivu yatakayomfanya alie na kukataa kutumia mkono ulioathirika. Pia mkono unaweza kupinda bila ya kuwapo uvimbe.

Kuzuia hali hiyo, inashauriwa kuepuka kumvuta au kumnyanyua mtoto kwa kumshika mikono, badala yake ashikwe chini ya kwapa au mwili mzima.

Daktari wa watoto katika Hospitali ya Regency, Rahim Damji anasema baadhi ya wazazi wanapenda kuwainua watoto kwa njia ya kuwaumiza pengine bila ya wao kujua.

“Mtoto chini ya miaka mitano mishipa, mifupa na misuli inakua haijakomaa. Mtoto akishaumia anashindwa kuuchezea huo mkono. Lakini tiba yake unaweza kumpa dawa za kuua maumivu,” amesema na kuongeza:

“Lakini maumivu yakiwa makali zaidi mzazi anashauriwa kwenda kwa daktari akamchunguze zaidi. Nawashauri wazazi wakitaka kuwanyanyua watoto wahakikishe wasiwanyanyue wakati mikono yao ikiwa imenyayuka juu.”

Amesema katika hospitali hiyo hupokea mtoto mmoja hadi wawili kwa wiki kutokana na tatizo hilo.

Katika tovuti ya elimu ya afya ya KidsHealth inaelezwa tatizo hilo ni jeraha la kawaida kwa watoto ambalo husababisha maumivu ya mkono na daktari anaweza kulitibu kwa urahisi.