Umemsikia Niyonzima Yanga? | Mwanaspoti

JANA, mashabiki wa Yanga waliwaona wachezaji wao wapya akiwemo akiwemo Balla Moussa Conte, Lassine Kouma, Mohamed Doumbia na mshambuliaji wa kati Andy Boyeli kwenye mechi hiyo ya kirafiki ambayo waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Rayon Sports mjini Kigali, Rwanda.

Katika mechi hiyo iliyomalizika kwa Yanga kushinda 3-1, Rayon Sports ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao ambalo Aziz Andambwile alijifunza. Niyonzima alisema ushindi huu ni ishara chanya, lakini kimsingi ni mtihani wa kuona jinsi kikosi kipya kinavyoendelea kushirikiana na kuboresha mbinu zao.

Lakini, nyuma ya ushindi huo nyota wa zamani wa Yanga, Haruna Niyonzima ameyataja mambo matatu ambayo ameyaona juzi, Ijumaa kwenye mechi ya kwanza ya kimataifa ya Yanga ambayo ilikuwa ikijipima ubavu huko Kigali, Rwanda dhidi ya wenyeji wao, Rayon Sports kwenye uwanja wa Amaholo.

“Nilishangazwa kuona jinsi wachezaji wanavyoweza kuungana haraka, kufanikisha mpangilio wa kocha (Folz), na kuonyesha kwamba hawahitaji muda mrefu kujua jukumu lao. Hii ni ishara kubwa kuwa kikosi hiki kinaweza kufanya makubwa zaidi kwa sababu kama maandalizi ya msimu ujao ndio kwanza yameanza,” amesema Niyonzima.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo unaonyesha kuwa Yanga inaweza kuendelea kuwa tishio ukanda wa Afrika Mashariki na kati kwani wachezaji wanapoelewana haraka, mashambulizi na ulinzi unakuwa imara.

Pili, fundi huyo ameeleza viwango vya kimwili na mbinu za kucheza. Niyonzima ambaye siku moja kabla ya mechi alipata nafasi ya kufanya mazoezi na kikosi cha Yanga, alisema kuwa wachezaji wapya kama Conte, Kouma na Doumbia walionyesha kasi, nguvu na ufundi.

“Nimeona wachezaji wakicheza kwa kasi hasa wanapokuwa kwenye eneo la wapinzani, wakibadilisha nafasi haraka, naamini bado kuna nafasi ya kuona zaidi kutoka kwao,” amesema.

Jambo la mwisho, ameeleza kuwa hali ya mashambulizi na mabao ilionyesha uwezo wa kikosi cha Yanga kushinda mechi kwa mtindo tofauti. Mabao ya Boyeli, Pacome Zouzoua yalionyesha wazi kuwa kikosi hiki kina wachezaji wenye uwezo wa kutimiza mashambulizi ya haraka.

Amesisitiza kuwa kikosi hiki kina wachezaji wengi wenye ubora mkubwa, na kwa kiwango alichokiiona, Yanga tena bila ya kuwa na wachezaji kama Mudathir Yahya na mebeki wake wa kati, Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ ambao wapo kwenye mashindano ya CHAN inaweza kuwa bora zaidi kadiri wachezaji wanavyoendelea kuwa pamoja.

“Mashabiki wa Yanga wana sababu ya kuendelea kuwa na matumaini. Kikosi hiki kina mchanganyiko mzuri wa uzoefu na wachezaji wapya wenye nguvu na mbinu. Ikiwa nidhamu na ushirikiano utaendelea, msimu huu unaweza kuwa wa kuvutia sana,” amesema.

Kocha Folz ameonyesha furaha yake baada ya mechi hiyo ya kirafiki, akibainisha kuwa wachezaji wameanza kuelewa maboresho ya mbinu za kikosi.

“Nimefurahi kuona wachezaji wanavyojibadilisha na kuanza kuelewa mpango wetu wa kucheza. Ushirikiano kati ya wachezaji wapya na waliopo ni muhimu, na nimeona dalili nzuri kuwa tunataka timu yenye nguvu, yenye kasi na ufanisi katika mashambulizi,” amesema Folz.

Folz ameongeza kuwa mechi ya kirafiki ilikuwa nafasi ya kupima nguvu za wachezaji na kujaribu mbinu mpya, akisema: “Tunahitaji kuendelea kuboresha mashambulizi ya pembeni na ushirikiano wa kati kati ya viungo na washambuliaji.”

Baada ya mechi hiyo ya kirafiki hesabu za Yanga kwa sasa ni kwenda Misri kwa ajili ya kuweka kambi ya muda mrefu zaidi kwa ajili ya kuendelea na maandalizi yake kabla ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara kuanza mwanzoni mwa mwezi ujao, Septemba.