Utaka adai angetoboa CHAN 2024

MSHAMBULIAJI wa zamani wa timu ya taifa la Nigeria, John Utaka amejipigia debe kwa kusema kama angepewa nafasi ya kuiongoza timu hiyo kwenye mashindano ya CHAN 2024, asingeishia hatua ya makundi kama ilivyo kwa Éric Sékou Chelle.

Nigeria chini ya Chelle imeweka rekodi mbovu, ikifungwa mechi mbili mfululizo katika hatua ya makundi, kwanza dhidi ya Senegal kwa bao 1-0, kisha Sudan kwa mabao 4-0, jambo ambalo limekera mashabiki na kuibua maswali kuhusu mbinu na kocha huyo.

Utaka mwenye historia ya kubwa ya uchezaji, alishinda Ligue 1 Ufaransa akiwa na Montpellier, FA Cup Uingereza akiwa na Portsmouth na Kombe la Kiarabu akiwa na Al Sadd.

“Naamini kuwa Nigeria inawachezaji wengi na wenye vipaji vikubwa, ishu ni namna ya kuwaunganisha wachezaji hao pamoja na kukupa matokeo, hilo ndio naamini lingeweza kunifanya tufike mbali,” alisema.

Utaka alizaliwa Enugu, Nigeria na kuanza maisha yake ya soka akiwa Enugu Rangers kabla ya kuhamia Misri, ambapo alijulikana sana akiwa na Ismaily, baada ya kufunga mabao 30 kwenye mechi 42.

Utaka aliichezea kwa mara ya kwanza Nigeria mwaka 2001, akicheza kwa mara ya kwanza dhidi ya Namibia na baadaye akajumuishwa kwenye kikosi cha Nigeria cha Kombe la Dunia 2002.

Mshambuliaji huyu pia alionesha kiwango kikubwa kwenye AFCON ya 2004, akifunga mabao mawili na kutoa asisti moja, akichangia Nigeria kushika medali ya shaba. Baada ya kutundika daruga, alifanya kazi katika klabu mbalimbali, ikiwemo Montpellier na Portsmouth.