TIMU ya Singida Black Stars inaendelea na maandalizi ya msimu ujao jijini Arusha chini ya Kocha Miguel Gamondi, huku uongozi ukimfuatilia kwa karibu winga El Mami Tetah anayeicheza Mauritania kwenye michuano ya CHAN 2024.
Tetah ni miongoni mwa nyota bora katika kikosi cha Mauritania kinachoshiriki michuano ya CHAN 2024 kikiwa kundi B na timu ya Taifa ya ‘Taifa Stars’, ambapo uwezo wake umezifutia timu mbalimbali ikiwemo Singida inayomfuatilia zaidi.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Tetah aliyezaliwa Novemba 12, 2001 amefanya mazungumzo ya awali na mabosi wa Singida jijini Dar es Salaam ikimhitaji, ingawa amewataka wasubirie kwanza hadi michuano ya CHAN iishe.
“Tumefanya mawasiliano tayari na menejimenti yake lakini wametuambia kwa sasa sio muda wa kumvuruga mchezoni kwa sababu ya ushiriki wake wa CHAN 2024, wametuomba tuwe na subra kwanza hadi pale michuano itakapoisha,” kilisema chanzo kutoka ndani ya timu hiyo.
Chanzo hicho kilisema baada ya kupewa ujumbe huo wameamua kusitisha mazungumzo hayo kwanza, japo tayari baadhi ya mabosi wa timu hiyo wameweka kambi jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea kufuatilia kwa ukaribu maendeleo yake kikosini.
Nyota huyo anayecheza winga ya kulia na kushoto kwa ufasaha, akicheza pia kiungo mshambuliaji, kwa sasa anaichezea AS Douanes (Nouakchott) aliyojiunga nayo Septemba 3, 2024, akitokea Alanyaspor iliyo jiji la Alanya Mkoa wa Antalya huko Uturuki.
Timu nyingine ambazo amecheza ni ACS Ksar Nouakchott ya kwao Mauritania na Arda Kardzhali ya Bulgaria, huku akichaguliwa pia nyota bora wa mechi kati ya Mauritania iliyoifunga Burkina Faso bao 1-0, katika michuano ya CHAN, Agosti 13, 2025.