Yanga yakosa mpiga kura Uchaguzi TFF

KLABU ya Yanga imekosa mjumbe atakayepiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa TFF unaofanyika leo jijini Tanga kwenye Hoteli ya Tanga Beach Resort.

Akizungumza jijini Tanga, Mwenyekiti Wa Kamati ya Uchaguzi TFF, Wakili Kiomoni Kibamba amesema Yanga imekosa sifa ya kupiga kura kwa sababu haijawakilishwa na Mwenyekiti kama kanuni zinavyoelezea.

“Kwa mujibu wa katiba ya TFF iliyofanyiwa marekebisho ya mwaka 2019, Inaeleza wazi mwenye haki ya kupiga kura ni Mwenyekiti wa Klabu na sio vinginevyo,” amesema Kiomoni.

Hatua hiyo inajiri baada ya Yanga kuwakikishwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Rodgers Gumbo tofauti na Mwenyekiti kwa mujibu wa kanuni hizo.

Mbali na Yanga iliyokosa wawakilishi wa kupiga kura, klabu nyingine za Ligi Kuu Bara ambazo hazikuwakilishwa na Mwenyekiti ni Coastal Union na Dodoma Jiji ambazo zimewakilishwa na Katibu Mkuu.

Kwa upande wa Simba, imewakilishwa na Mwenyekiti wa timu hiyo, Murtaza Mangungu.