Zawadi kwenye paketi za vyakula hatari kwa watoto

Dar es Salaam. Wakati matumizi ya bidhaa za vyakula vya kwenye paketi vinavyouzwa pamoja na zawadi ndogo, hasa kwa watoto yakiongezeka nchini, wataalamu wa afya wanaonya wakitaka uwepo umakini kwa watumiaji, kwani zawadi hizo zinaweza kusababisha madhara ya kiafya na kijamii.

Zawadi hizo mara nyingi ni bidhaa za kuchezea au vifaa vidogo vya plastiki (kama vile mwanasesere, gari, gitaa), vinavyowekwa ndani ya paketi, hususani za vitafunwa.

Licha ya kuwa zawadi hizo hutumika kama mbinu ya kuvutia biashara, wataalamu wa afya na malezi ya watoto wanaonya kuhusu madhara yake kwa afya na maisha ya kijamii.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Agosti 16, 2025, Namala Mkopi, daktari mbobezi wa uangalizi wa watoto ICU, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) amesema katika kipindi cha miezi minane, wamepokea watoto watano waliomeza vitu vyenye asili ya plastiki na watatu kati ya hao walifariki dunia.

Baadhi ya hao amesema vitu hivyo vilikwama kwenye njia ya hewa.

“Kuna wengine wanaletwa wamechoka kabla hawajafikia hatua ya kusaidiwa wanapoteza uhai. Hatujui walimeza kitu gani wakati mwingine ni vigumu, si wote wanaofanikiwa, wengine hawafiki hospitalini na hujui tatizo lilikuwa nini,” amesema.

Kutokana na hilo, amewashauri wazazi kuwakinga watoto kabla ya kupata athari hizo.

Mkazi wa Mtoni kwa Aziz Ally, Iddi Ahmad anasema mtoto wake akiwa shuleni alimeza kipande cha plastiki kutoka kwenye zawadi aliyopata kwenye paketi ya kitafunwa, kikaziba njia yake ya hewa.

“Alipelekwa hospitali ya awali ikashindikana, baadaye walimpeleka Temeke nako ikashindikana akawekewa mashine ya oksijeni wakambeba kwenye ambulensi mpaka Muhimbili. Alifanyiwa uchunguzi madaktari wakakitoa kiplastiki. Nawashauri wazazi wawe makini na watoto wao,” amesema.

Akimzungumzia mtoto huyo, Dk Namala amesema alipokewa Muhimbili na kupewa matibabu baada ya huduma ya dharura aliyopata Temeke iliyosaidia kuokoa maisha yake.

Dk Namala anashauri mzazi, mlezi au mtu yeyote anapohisi mtoto amemeza kitu amuwahishe kwenye hospitali kubwa yenye wataalamu na vifaa, ili apatiwe huduma.

“Anahitaji kupatiwa oksijeni haraka iwezekanavo ili asipoteze iliyopo mwilini akapoteza maisha. Ukianzia hospitali za chini utalazimika kwenda za juu, hivyo unamchelewesha mgonjwa,” amesema.

Mzazi aliyejitambulisha kwa jina la Winarix kwenye mtandao wa kijamii akizungumzia suala hilo amesema: “Hii iliwahi mtesa mwanangu sitakaa nisahau. Alichukua hicho kidude akakisokomezea puani, nilimpeleka hospitali akapelekwa chumba cha upasuaji, sina hamu navyo.”

Inaelezwa bidhaa hizo pia huchochea ulaji wa vyakula visivyo na lishe bora kwa watoto, kwani wengi huzinunua ili kupata zawadi.

Kwa kufanya hivyo, huchangia ongezeko la ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi, jambo linaloweza kusababisha unene uliokithiri, matatizo ya meno na hatari ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza wakiwa watu wazima.

Kisaikolojia mtoto hujengewa dhana kwamba kila chakula lazima kiambatane na zawadi au burudani, hivyo kuvuruga mafunzo ya malezi kuhusu ulaji bora na kuimarisha utegemezi wa kisaikolojia kwenye bidhaa za viwandani.

Si hivyo tu, mzazi anaposhindwa kununua bidhaa hizo, migogoro ya kifamilia huibuka kutokana na watoto kulilia zawadi.

Mtaalamu wa saikolojia, Charles Nduku amesema vyakula hivyo kutokana na kuwa na chumvi nyingi pamoja na sukari, ni rahisi kutengeneza uraibu kwa watoto.

“Akilini mwake anakuwa anavifikiria zaidi na kutamani kula mara kwa mara, hiyo inaanza kumtoa kwenye kupenda vyakula vingine vinavyohitajika mwilini.

“Ataanza kuvichukia, anapunguza kasi ya kula na madhara yake ni unene kupita kiasi na athari za baadaye,” amesema.

Meneja mradi wa afya ya mama na mtoto na mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Word Vision, Dk Daud Gambo amesema viburudisho hivyo lazima viangaliwe kwa makini kama vina lishe au manufaa yoyote.

“Ni biashara watu wanapata hela lakini haisaidii chochote, juenda kina mzio kwa mtoto au anayetumia, kinachofanya zisiharibike pia kinaweza kudhuru mtoto, hakimuondolei njaa, hakimpi nguvu wala vitamini inawezekana ni kitamu kwake ila hakimsaidii zaidi ya kumuathiri,” amesema.