KIKOSI cha Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Azam FC kipo Kigali, Rwanda kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa 2025-2026 na kuanzia Jumanne ijayo itakuwa na kazi moja ya kutesti mitambo kwa ajili ya mechi za kimataifa.
Mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Bara 2013-2014, ilianza kambi ya maandalizi jijini Dar es Salaam kabla ya kwenda Karatu, Arusha na ikiwa huko ilicheza mechi kadhaa za kujipima nguvu, kisha kupaa hadi Kigali na itakuwa na kazi ya kujipima kwa mechi za kimataifa kabla ya kuingia mzigoni CAF.
Azam imepangwa kuvaana na Al Merrikh Bentiu ya Sudan Kusini katika mechi za raundi ya kwanza itakayoanza katikati ya mwezi ujao na kama itavuka salama hapo itakutana na mshindi wa mechi kati ya AS Port ya Djibouti na KMKM ya Zanzibar.
Ikiwa Kigali, Azam itacheza mechi nne za kimataifa katika michuano maalumu ya Inkera Y’abahizi, waliyoalikwa na wenyeji wao APR ya Rwanda.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mitandao ya kijamii ya klabu hiyo iliyomaliza nafasi ya tatu katika Ligi Kuu msimu uliopita nyuma ya mabingwa Yanga na Simba, itacheza mechi hizo nne za kimataifa kabla ya kurejea nchini mwishoni mwa mwezi huu kujiandaa na msimu mpya.
Azam itaanza kibarua Jumanne ya Agosti 19 dhidi ya Polisi Rwanda, kisha Alhamisi ya Agosti 21 itaumana na AS Kigali na siku tatu baadae itavaana na wenyeji wa APR na kumalizia ziara ya nchini humo kwa kucheza na Vipers ya Uganda Ijumaa ya Agosti 29.
Azam inayonolewa na kocha kutoka DR Congo, Florent Ibenge ina kibarua cha kusaka kutinga makundi katika michuano ya CAF kwa mara ya kwanza, kwani haijawahi kufanya hivyo tanvgu ilipoanza kushiriki michuano ya kiimataifa, ambapo msimu uliopita ilitolewa raundi ya kwanza kwa kufunga jumla ya mabao 2-1 na APR, ikianza na ushindi wa bao 1-0 nyumbani na kulala ugenini mabao 2-0.
Katika kuonyesha kuwa safari hii Matajiri hao wa Chamazi wamejipanga wameshusha nyota wa maana sambamba na benchi lenye vichwa adimu chini ya Ibenge aliyekuwa akiinoa Al Hilal ya Sudan, akiwa pia na rekodi tamu katika michuano ya CAF kuanzia ngazi ya klabu hadi timu za Taifa.
Baadhi ya nyota wapya waliosajiliwa na kutambulishwa Azam FC ni moja na Japhte Kitambala, Sadio Kanoute, makipa Issa Fofana na Aishi Manula aliyerejea nyumbani kama ilivyo kwa Edward Manyama na Himid Mao ‘Ninja’.
Wengine ni Watunisia, Ihmidi Barakat na Ben Zitoun Tayeb, Papa Doudou Diallo, Muhsin Malima na wengine ambao wameungana na mastaa waliokuwapo msimu uliopita na kuifanya Azam kumaliza ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, licha ya kung’olewa mapema katika Kombe la FA.