::::::::
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema ujenzi wa madaraja katika barabara kuu ya Dar es Salaam–Lindi (T7) unaendelea kwa kasi kupitia mpango wa dharura wa CERC, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa zaidi ya shilingi bilioni 114.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi katika madaraja ya Somanga Mtama, Kipwata na Mkereng’ende, Mhandisi Besta amesema miradi hiyo imefikia asilimia 75 ya utekelezaji na itakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo kwa mikoa ya Lindi na Kanda ya Mashariki ya Pwani ya Tanzania.
“Nimefanya ukaguzi na kuona ujenzi unaendelea vizuri. Namshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha fedha hizi zinapatikana ili kuondoa adha za mvua na dhoruba zilizokuwa zikisababisha barabara kutopitika,” alisema Mhandisi Besta.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, mvua kubwa ziliharibu baadhi ya madaraja na makaravati kwenye barabara hiyo, hali iliyosababisha usumbufu mkubwa kwa wasafirishaji na wananchi.
Aidha, ameeleza kuwa kazi za makaravati pia zimefikia hatua ya mwisho ambapo 11 kati ya 18 tayari yamekamilika, na akatoa maelekezo kwa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi kuongeza usimamizi ili ujenzi ukamilike kwa wakati.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Lindi, Mhandisi Emil Zengo, amewahakikishia wananchi na wasafirishaji kwamba madaraja hayo yatakamilika kwa wakati kwa kuzingatia vigezo na taratibu za kimkataba.
“Niwatoe wasiwasi Watanzania wote kwamba madaraja haya yatakamilika kwa muda uliopangwa, na tunashukuru kupata sapoti ya karibu kutoka kwa Mtendaji Mkuu,” alisema Mhandisi Zengo.
Miradi hiyo inatajwa kuongeza ufanisi wa barabara ya kutoka Dar es Salaam hadi Lindi na kuchochea maendeleo ya uchumi katika Kanda ya Mashariki ya Pwani ya Tanzania kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao na bidhaa kutoka mikoa ya kusini.