Chadema inazalisha vyama ‘maadui’, CCM inavirutubisha

On Liberty ni insha ya mwanafalsafa wa Uingereza, John Stuart Mill. Insha hiyo ilichapwa kama kitabu mwaka 1859. Karne moja na miaka 66 imepita, tangu chapisho hilo lilipokamilishwa.

Ndani ya On Liberty, Mill aliandika: “If you don’t know the other side’s argument, you really don’t know much of your own, either.” – “Kama hujui hoja za upande wa pili, unakuwa hujui vizuri hoja zako pia.”

Tatizo kubwa la vyama vya siasa ni kila chama kudhani kinajua kila kitu, kiasi cha kutotaka kushawishiwa na hoja za upande wa pili. Viongozi wa kisiasa wanajiona wanajua yote wanayopaswa kujua. Hawaambiwi kitu kipya.

Ugonjwa huu wa kuamini unajua kila kitu na kuziba masikio dhidi ya mawazo mapya, unaitwa ujuaji. Miaka 33 tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, upinzani unaendelea kupepesuka. Sababu kubwa ni ujuaji.

Kama NCCR-Mageuzi iliyokuwa tishio kisiasa, mafahari wake wa pande mbili wangepata nafasi ya kusikilizana, pengine chama hicho kingekuwa na nguvu ileile hadi sasa. Ubishani na kupingana bila kupeana nafasi ya kusikilizana, ni sumu inayoua upinzani.

Hoja ya aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Augustino Mrema ilikuwa nini? Mtazamo wa Katibu Mkuu wake, Mabere Marando, ulieleweka dhidi ya waliompinga? Badala ya kuzungumza kama timu moja inayotafuta kuimarisha afya ya taasisi, walichagua kunyukana, chama kikaangukia korongoni.

Jini gani alisimama katikati mwaka hadi mwaka, Zitto Kabwe na wenzake, wakashindwa kuelewana na wenzao Chadema, kisha wakafukuzwa? Zitto, Profesa Kitila Mkumbo, Samson Mwigamba, walisikilizwa inavyotakiwa au walikamiwa kuoneshwa cha mtema kuni?

Swali hilohilo, litumike kumwelekea Chacha Wangwe, kabla ya mauti kufika. Halafu, liwaelekee Dk Willibrod Slaa, Fredrick Sumaye na wengine walioondoka Chadema kwa manung’uniko kwamba mambo hayakuwa sawa kwenye chama hicho. Walisikilizwa sawasawa? Nao waliwasikiliza waliowapinga?

Kuisogelea hali ya sasa, turukie mtifuano wa Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, akiwa na kundi lake, dhidi ya mtangulizi wake, Freeman Mbowe, na timu yake. Ni wakati gani kila upande ulijishughulisha kuelewa hoja za wenzao wa upande wa pili? Kilichoonekana kilikuwa kurushiana mafatuma bila huruma, wala kutambua wao ni msingi wa taasisi yao.

Kisha, Mbowe akashindwa uchaguzi kwenye chama baada ya kuvunjiwa heshima kwa kiwango kikubwa, na kung’oka kwake kukazalisha waasi wa uongozi mpya waliojiita G55.

Viongozi wapya Chadema na G55, kila upande haukuwa na muda wa kumsikiliza na kumwelewa mwenzake. Walichagua kusemana kupitia chaneli za umma.

Zitto, Profesa Kitila na mwenzao, Samson Mwigamba, waliondoka Chadema na kuanzisha kituo kipya cha kazi, chama cha ACT-Wazalendo. Uchaguzi Mkuu 2015, ACT walipata mbunge mmoja tu (Zitto Kabwe – Kigoma Mjini) na Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Baada ya Uchaguzi Mkuu 2015, Rais wa Tano, Dk John Magufuli, aliidhoofisha ACT kwa kuwatwaa viongozi wake, Profesa Kitila, aliyemteua kuwa Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, vilevile aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT, Anna Mghwira, alimfanya kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

ACT ilipata nguvu mpya mwaka 2019, kwa mavuno iliyoyapata kupitia mgogoro wa Chama cha Wananchi (CUF). Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Cuf, Seif Sharif Hamad, alihamia ACT na timu kubwa iliyokuwa inamuunga mkono. Nguvu kubwa ya Seif na wenzake, iliiwezesha ACT kuwa chama imara, hususan Zanzibar.

Kwa hatua ambayo ACT ipo leo, haiwezi kusahaulika kuwa mwanzo wake ni Chadema. ACT ni chama kilichozaliwa kutokana na mgogoro wa Chadema, kikapata nguvu kupitia mpasuko wa CUF. Viongozi, wanachama na wafuasi wa ACT, kwa sehemu kubwa walikuwa viongozi na wafuasi wa Chadema na Cuf.

Mnyukano wa pande mbili za shilingi, baina ya Mbowe na Lissu, ukatengeneza G55. Kushindwa kusikilizana kati ya G55 na uongozi mpya Chadema, ukasababisha wimbi kubwa la viongozi waliohamia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma).

Ghafla, Chaumma kilichoasisiwa mwaka 2013 kikiwa hakina msuli wa kupambana kisiasa, sasa kimekuwa kipya na chenye ukwasi.

Chaumma ya sasa siyo ile ya kusuasua ya Hashim Rungwe peke yake. Chaumma yenye menejimenti mpya, na sehemu kubwa ya viongozi wakiwa wametokea Chadema, imekuwa taasisi yenye utambulisho wa tofauti kisiasa. Chaumma mpya inawaza viti vya ubunge, inapiga hesabu ya kuwa chama kikuu cha upinzani Tanzania.

Wakati huohuo, ACT nao kikokotoo chao cha Uchaguzi Mkuu 2025 ni kupata matokeo bora Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni ama kushinda uchaguzi au kutoka wa pili visiwani, wakati huohuo watoke namba mbili upande wa Muungano na kuongoza upinzani ndani na nje ya Bunge.

ACT wana mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni Luhaga Mpina, ambaye ni mbunge wa zamani wa Kisesa, kwa tiketi ya CCM. Mpina alikatwa kwenye mchakato kupata wagombea ubunge CCM. Amehamia ACT, sasa anagombea urais.

Mpina sasa amekuwa rutuba kutoka CCM, inayokwenda kuistawisha ACT. Mpina atazunguka nchi nzima akinadi mabaya ya CCM na Serikali, huku akiuangukia umma umchague awe Rais na wawapigie kura wagombea ubunge wa ACT. Kwa namna yoyote, ACT watanufaika kupitia Mpina.

Utayari wa CCM kuingia kwenye uchaguzi bila ushiriki wa Chadema, ni jambo lingine ambalo linavistawisha vyama vya ACT na Chaumma, ambavyo kiasili, uzao na nguzo yao kisiasa imetokea Chadema.

ACT na Chaumma vinajiona kwa sasa vinatembea mwendo salama, maana ipo fursa ya kuwa vyama vya upinzani kwa sababu Chadema hawashiriki Uchaguzi Mkuu 2025.

Hivi sasa, kwa Chadema kutoshiriki uchaguzi, Chaumma na ACT kushiriki, pamoja na vyama vingine, kumesababisha hali ya vyama vya upinzani kushambuliana wao kwa wao, badala ya kuelekeza shabaha yao kwa CCM.

Ukiwatazama viongozi wa Chaumma wakiwa kwenye majukwaa ya kisiasa, unaweza kudhani wapinzani wao ni Chadema. Kadhalika, ACT, wanapambana kujibu hoja za Chadema ili kutetea hoja zao za kushiriki uchaguzi, kuliko kuikabili CCM.

Angalau Mpina, tangu amejiunga ACT, shabaha yake moja kwa moja ni CCM. Chadema wao wamekuwa njiapanda, hawajui shabaha yao hasa iende wapi.

Mara mahakamani kutetea Lissu kwamba kesi yake ya uhaini ni batili, au shauri la mali za Chadema lililofunguliwa na kada wao kuwa ni mpango wa CCM.

Wakigeuka upande mwingine, Chadema wanageuka washereheshaji wa hoja za makada wa CCM wanaonung’ukia hali ya mambo inavyokwenda, ambao ni Humphrey Polepole na Josephat Gwajima. Wakati huohuo wanaiponda ACT kushiriki uchaguzi bila mabadiliko ya sheria.

Chadema wanakwenda sawa na Chaumma, kwamba ni wasaliti na wenye tamaa ya fedha na madaraka. Kitendo cha Chadema kuwa na matawi mengi ya ugomvi, kinasababisha nishati yao itumike zaidi, wakati huohuo CCM wao wanajielekeza kwenye Uchaguzi Mkuu 2025.

Ndani ya miaka 33 ya uhai wa Chadema, inaweka rekodi ya kuzalisha vyama vipya, vinavyogeuka maadui na kushambuliana majukwaani, wakati CCM inavirutubisha kidogo, lakini kwa sehemu kubwa inanufaika jinsi Chadema inavyogawanyika na kujijengea mahasimu wapya kisiasa.