Dk Biteko: Tunajivunia mchango wa viongozi wa dini

Geita.Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini ili kuchagiza maendeleo na ustawi wa wananchi.

Dk Biteko amesema hayo leo Jumapili Agosti 17, 2025 wakati akimwakilisha Makamu Rais, Dk Philip Mpango katika maadhimisho ya miaka 125 ya Ukristo na Uinjilishaji katika Parokia ya Kome, Jimbo Katoliki la Geita.

“Niseme Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi zote za dini katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na hii ni kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo,” amesema Dk Biteko.

“Serikali inafarijika kutokana na mchango wa taasisi za dini kuwaletea wananchi maendeleo katika maeneo yao.”

Sambamba na ibada hiyo ya Jubilei, Dk Biteko ameongoza harambee ya ujenzi wa mradi wa maji kwa ajili ya huduma katika makazi ya masisita, Parokia ya Kome.

Akizungumza baada ya Misa Takatifu, Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, Mhasham FLavian Kassala ameuombea baraka mchakato wa uchaguzi ili Tanzania iwapate  viongozi sahihi baada ya uchaguzi mkuu utakaofanyika  Oktoba 29 mwaka huu.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Askofu Kassala amemshukuru pia Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa ushirikiano wanaoutoa kwa taasisi za dini ambazo zimekuwa chachu ya maendeleo katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema huduma ya majisafi na salama katika Kisiwa cha Kome bado ni changamoto hivyo, ameiomba Serikali kufanikisha mpango wa upatikanaji wa majisafi kwa wakazi wa eneo hilo.

“Pamoja na kwamba hapa ni kisiwani tumezungukwa na maji, huduma ya majisafi bado ndogo na wananchi wenye uwezo wa kupata maji ni wachache,” amesema Askofu Kassala.

Amesema kanisa liko katika jitihada za kusogeza huduma za jamii kwa kuongeza watawa zaidi watakaotoa huduma za jamii, hivyo, wanahitaji huduma za haraka.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Dk Biteko amesema Serikali itafanya upembuzi ili kuhakikisha huduma hiyo ya maji inapatikana ili kuhakikisha watawa wanayapata.

Amewaomba wakazi wa Kome kuzidisha moyo wa ushirikiano sambamba na kuboresha mazingira na kupanda miti ili kulinda na kurejesha uoto wa asili.

Pia, amechangia Sh10 milioni katika harambee hiyo huku akiwasilisha mchango wa Sh50 milioni uliotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, ikiwa ni sehemu ya kufanikisha azma ya kufanikisha upatikanaji wa huduma ya maji katika makazi ya watawa hao wa Kome.

Awali, akihubiri katika ibada ya maadhimisho ya miaka 125 tangu kuanzishwa kwa utume katika Parokia ya Kome, Askofu Mkuu wa Jumbo Kuu la Mbeya, Mhasham Gervas Nyaisonga amewataka waumini kushikamana, kuvumiliana na kujenga maelewano kati yao.

“Tunapoadhimisha miaka 125 ya utume tujitahidi kuelewa kuwa, tunatakiwa kustawisha umoja na utulivu miongoni mwetu, sisi ni wadhaifu tuna mapungufu, tumgeukie Mungu na kuomba nguvu,” amesema Askofu Mkuu Nyaisonga.

Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao, Nyaisonga amewataka wakatoliki kufanya maombi maalumu kwa saa 24 kuanzia Agosti 23-24 mwaka huu ili kufanikisha uchaguzi wa amani utakaowezesha kupatikana viongozi bora.