Kinda wa Kitanzania anayekipiga Ceu Ciutat Meridiana ya Hispania, Fahmar Santos amesema ripoti ya daktari inaeleza atakaa nje ya uwanja kwa takribani miezi tisa sawa na msimu mzima, baada ya kufanyiwa operesheni ya goti la mguu wa kulia.
Mwishoni mwa msimu huu, kinda huyo (21) alipata jeraha la goti na Jumamosi, Agosti 8 mwaka huu, alifanyiwa operesheni na kwa sasa ameanza kuufanyia mguu mazoezi mepesi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Santos alisema licha ya kupata majeraha, msimu uliopita ulikuwa mzuri kwake, akifunga mabao 15 kwenye mechi 20 za Ligi Daraja la Nne Hispania, maarufu Catalunya.
“Msimu wa kwanza sikufanikiwa kucheza ligi ila msimu wa pili nashukuru Mungu mambo mazuri, ila msimu huu umekuwa mzuri sana nimefunga mabao 15 katika mechi 20, ila sikubahatika kumaliza msimu vizuri kutokana na majeraha,” alisema Santos na kuongeza:
“Huu ni msimu wangu wa mwisho, nilisaini mkataba wa miaka minne, kwa hiyo kuna ofa nimepata ila bado nazichekecha kuangalia nzuri, zikiwa tayari nitakujuza naenda wapi.”
Fahmar alijiunga na timu hiyo msimu wa 2022/23 akitokea Ruvu Shooting aliyohudumu nayo kwa misimu miwili (2019/20 na 2020/21). Pia Zanzibar alicheza Zanzibar Real Kids, ambako ndipo alipozaliwa.