KIUNGO mshambuliaji wa Taifa Stars, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameendelea kuonyesha ubora alionao katika mashindano ya CHAN 2024 baada ya jana usiku kubeba tuzo ya pili ya mchezaji bora wa mechi dhidi ya Afrika ya Kati ikiwa ni mechi ya mwisho ya Kundi B iliyopigwa Kwa Mkapa.
Katika mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa suluhu, Fei toto alipiga mashuti matano, huku mawili yakilenga lango mbali na hilo aliibeba Stars katika eneo la kiungo na kuifanya kuwa na umiliki wa mpira kwa asilimia 68.
Fundi huyo wa Kizanzibar, alianza kubeba tuzo za mchezaji bora wa mechi katika ufunguzi tu wa michuano hiyo ambapo aliisaidia Stars kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Burkina Faso.
Akiongelea juu ya tuzo hiyo, Fei toto alisema: “Nashukuru Mungu kwa matokeo haya, na pia kwa kupewa tuzo ya mchezaji bora wa mechi kwa mara nyingine tena hii inamaana kubwa sana kwangu na timu kwa ujumla.”
Nyota huyo wa Azam aliongeza kwa kusema; “Tumemaliza hatua ya makundi vizuri, na sasa hesabu zetu ni robo fainali, nashukuru Watanzania kwa sapoti yao bado tunawahitaji katika hatua inayofuata.”
Katika orodha ya wachezaji ambayo wamezikusanya sana tuzo za mchezaji bora wa mechi, anayeongoza ni Ramandimbisoa Michel Toldo wa Madagascar, akibeba mara tatu, moja zaidi kwa Fei toto.
Wachezaji wengine waliobeba mara mbili ni Abdelrazig Taha Yagoub Omer wa Sudan na Alhassane Bangoura wa Guinea. Kwa Stars wachezaji ambao wamebeba tuzo hiyo mbali na Fei toto ni Clement Mzize na Mudathir Yahya kila mmoja akibeba mara moja.