Dar es Salaam. Kihoro kimetawala miongoni mwa watiania walioshiriki kura za maoni za ubunge na uwakilishi katika Chama cha Mapinduzi (CCM), wakati vikao vya juu vya uteuzi vikianza.
Swali kuu miongoni mwao ni iwapo walioongoza kwenye kura za maoni ndio watakaoteuliwa, au wengine wanaweza kuinuliwa na kuwa wateule kutokana na sababu mbalimbali.
Kitendawili hiki kitateguliwa ndani ya siku saba za mfululizo wa vikao vya juu, vilivyoanza jana Agosti 15, 2025 ilipoketi Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) kuwajadili watiania ubunge na uwakilishi wa makundi viti maalumu.
Baada ya kuwajadili kamati hiyo, inatoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu kwa Tanzania Bara, kwa upande wa Zanzibar, itayapeleka kwa kamati maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa visiwani humo.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, jana Agosti 16, 2025 kikao cha Sekretarieti ya Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, kimechambua majina ya wagombea ubunge na uwakilishi wa jimbo na viti maalumu kwa ajili ya maandalizi ya vikao vya uteuzi.
Hatua hiyo inakuja baada ya chama hizo kukamilisha uteuzi wa udiwani uliofanywa na Agosti 13, 2025 na halmashauri kuu ya mikoa, ulioacha vicheko kwa watiania walioongoza katika kura za maoni na vilio kwa wachache ambao hawakuteuliwa.
Sasa ni zamu ya watiania wa ubunge, uwakilishi wa majimbo na viti maalumu kusubiria hatima yao kupitia vikao vikavyohitimishwa na halmashauri kuu ya taifa itakayofanya uteuzi Agosti 22.
Kutokana na kauli zilizowahi kutolewa na viongozi wa juu, vikao hivyo vinatarajiwa kufanya kama ilivyokuwa kwa watiania wa udiwani ambao asilimia kubwa walioongoza kura za maoni wameteuliwa.
Licha ya watiania hao kuvuka vingingi kadhaa kuanzia ngazi ya awali ya wilaya, mkoa, kamati kuu na wajumbe waliowapigia kura za maoni, kumekuwepo malalamiko na madai ya uwepo wa vitendo vya rushwa na vingine vya kimaadili kwenye baadhi ya maeneo.
Vikao hivyo vya uteuzi vitakavyozingatia hali hiyo, vitafanyika kipindi ambacho tayari Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imefungua dirisha la uchukuaji na urejeshaji wa fomu za udiwani na ubunge kuanzia Agosti 14 hadi 27.
Kampeni zitaanza Agosti 28 hadi Oktoba 28 kabla ya upigaji kura Jumatano Oktoba 29, 2025.
Kwa upande wa Zanzibar, watiania watalazimika kuvuka kigingi Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar itakayoketi Agosti 17, 2025 kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Kamati Kuu kuhusu wanaoomba nafasi ya ubunge na uwakilishi wa jimbo na viti maalumu.
Wakati Agosti 18, 2025 kitaketi kikao cha Sekretarieti ya Kamati Kuu ya CCM kuchambua majina hayo kwa ajili ya maandalizi ya vikao vya kitaiafa.
Agosti 20, 2025 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa itaketi kufikiria na kutoa mapendekezo yake kwa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kuhusu waombaji hao, kabla ya uteuzi wa mwisho utakaofanyika Agosti 22, 2025.
Kwa kifupi watiania wa ubunge na uwakilishi watakaoteuliwa watakuwa na siku tano pekee za kuchukua na kujza fomu za za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) zilizoanza kutolea kuanzia Agosti 14 hadi Agosti 27, siku ya uteuzi ya watiania urais na ubunge.
Michujo ya ndani ya CCM si jambo jipya. Katika chaguzi zilizopita, kumekuwa na mjadala mkubwa juu ya dhima ya kura za maoni dhidi ya uamuzi wa vikao vya uteuzi.
Mwaka 2010 na 2015, kulikuwepo na malalamiko ya baadhi ya watiania walikongoza kura za maoni lakini wakapitwa na wale waliokuwa nyuma yao, kwa maamuzi ya vikao vya juu vya chama.
Mfano, mwaka 2010 kulisikika malalamiko kutoka baadhi ya majimbo ya Arusha na Mwanza, ambapo walioshinda kura za maoni hawakupitishwa na chama.
Mwaka 2015, hali kama hiyo ilijitokeza tena katika baadhi ya majimbo ya Dodoma na Morogoro.
Mifano hii inaonyesha kuwa kura za maoni ndani ya CCM mara nyingi ni kipimo cha awali cha kukubalika kwa mgombea, lakini si dhamana ya moja kwa moja ya uteuzi.
Kwa sasa, watiania wa ubunge na uwakilishi wako kwenye wakati mgumu. Wengi wao tayari wametumia rasilimali nyingi kusaka kura za maoni. Wamejenga mitandao ya kisiasa, wamewasiliana na wajumbe, na wengine wanakabiliwa na tuhuma za kutumia fedha kama mbinu ya kushawishi kura.
Sasa macho na masikio yao yote yameelekezwa kwa vikao hivi vya kitaifa ambavyo havitegemei kura pekee, bali huangalia mambo mengine kama uwezo wa mgombea kushinda jimbo, historia yake ya kisiasa, nidhamu kwa chama na nafasi ya kuimarisha umoja ndani ya CCM.
Kwa maneno mengine, kura za maoni ni mwanzo tu wa safari, lakini si mwisho wa ndoto.
CCM imekuwa ikisisitiza mara zote kuwa vikao vya juu vina mamlaka ya mwisho ya kufanya maamuzi kwa masilahi mapana ya chama, si kwa matokeo ya kura za maoni pekee.
Kwa upande mmoja, kura za maoni hujenga imani kwa wanachama kwamba sauti yao inasikika. Lakini kwa upande mwingine, vikao vya juu vinapokuwa na mamlaka ya kubadili matokeo, husababisha hisia za kukatishwa tamaa kwa wagombea na wapiga kura wa ndani ya chama.
Akizungumza Agosti 9, 2025, wakati akitoka kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuwania nafasi ya urais wa Tanzania, Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan, aliwataka wanachama kuwa wamoja baada ya mchakato wa uteuzi kukamilika.
“Kama ilivyo desturi yetu ya CCM, mchakato wa uteuzi unapoisha na makundi nayo yaishe na ushindani ndani ya chama nao uishe, tunarudi kuwa kitu kimoja ili tuingie kwenye uchaguzi tukiwa wamoja na mshikamano,” alisema.
Pia Rais Samia alisema ni muhimu kudumisha desturi hiyo na vilevile wajitokeze katika maeneo yao kuwaunga mkono wagombea wao wanapokwenda ofisi za INEC kuchukua fomu za kuwa wagombea.
“Hawa ni wagombea wa chama chetu na sote tupo kwenye timu moja, hivyo twendeni kwa umoja na mshikamano kama timu ili tuhakikishe ushindi wa kishindo kwa chama,” alisema Samia.