Kilimanjaro ya Sweden yatwaa ubingwa wa bonanza Ubelgiji

TIMU ya soka ya Watanzania, Kilimanjaro iliyopo Sweden imetwaa tena kwa mara ya nne mfululizo ubingwa wa Kombe la Bonanza la Serengeti katika michuano iliyofanyika kati ya Agosti 15-16 jijini Antwerp, Ubelgiji.

Kilimanjaro ilitetea ubingwa huo baada ya kuifunga timu nyingine ya Watanzania kutoka Uingereza iitwayo Leeds Swahili kwa mabao 2-1 katika mchezo mkali wa fainali.  Mabao ya Kilimanjaro yalifungwa na Feisal Amir na Fryad Sabri, lile la kufutia machozi la Leeds likifungwa na Murtaza Fuad.

Hii ni mara ya tatu kwa timu hizo kukutana katika mechi ya fainali.

Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Jestas Nyamanga, alimkabidhi kombe la ubingwa nahodha wa Kilimanjaro, Abbas Bachu, ambaye naye alimkabidhi Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi na kuibua shangwe kwa mashabiki wa timu hiyo. Kilimanjaro inashiriki Ligi Daraja la Sita ya Sweden katika mfumo wa madaraja saba.

Michuano hiyo iliyofanyika kwa mara ya nne tangu mwaka 2021 na kudhaminiwa na Benki ya NBC na kampuni ya ASAS, zote za Tanzania, huandaliwa kwa lengo la kuwaunganisha Watanzania ughaibuni, kukuza vipaji vya soka na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Mkurugenzi wa Diaspora kutoka Tanzania, Salvatory Mbilinyi; Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Caroline Chipeta; na Mabalozi wa Kenya, Sudan Kusini na Somalia nchini Ubelgiji nao walishuhudia.

Jumla ya timu 15 za Watanzania na watu wa Afrika Mashariki waishio Ulaya zilimenyana.

Waandaaji Tanzania walikuwa na timu 10 kutoka Sweden, Ubelgiji, Uholanzi, Uingereza, Scotland, Ujerumani na Ufaransa, huku Burundi ikiwa na timu tatu na moja moja kutoka Rwanda na Somalia.