Kilio cha watumiaji barabara ya Kilwa, Serikali yatoa kauli

Dar es Salaam. Ikiwa imepita miezi mitano tangu kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa barabara ya Kilwa, kipande kutoka Mbagala hadi Kongowe, watumiaji wa barabara hiyo wamelalamikia adha wanayokutana nayo, kwa kile wanachoeleza kuwa imeelemewa na wingi wa magari kuliko uwezo wake.

Machi 19, 2025, Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam ilisaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe, yenye urefu wa kilomita 3.8 kwa kiwango cha lami.

Mradi huo unatarajiwa kugharimu Sh54 bilioni na utatekelezwa kwa kipindi cha miezi 15 kuanzia siku uliosainiwa mkataba huo. Hata hivyo, ujenzi huo haujaanza.

Barabara hiyo, inayounganisha Dar es Salaam na mikoa ya Pwani ikiwamo Lindi, kwa sasa inapitisha idadi kubwa ya magari yenye uzito tofauti, hali inayosababisha msongamano ambao wakati mwingine unatokana na baadhi ya magari, hasa ya mizigo, kuharibika au kukwama njiani.

Si hivyo tu, ajali za mara kwa mara zimekuwa zikichangia kipande cha Mbagala-Kongowe kutopitika, hasa nyakati za asubuhi na jioni, hali inayoleta adha kwa watumiaji na wakati mwingine kuwaathiri kiuchumi.

Miongoni mwa matukio ya ajali ni ile iliyotokea Agosti 14, ambapo gari la abiria lilifeli breki na kusababisha kuwakanyaga waendesha bodaboda waliokuwa wanapita kwenye barabara ya mchepuko wakikwepa foleni ya barabara kuu.

“Hapa imeshakuwa kama eneo la machinjioni, ni ajali kila kukicha. Juzi watu wamesagwa na Eicher, na hilo ni tukio la siku moja, lakini tunazishuhudia nyingi. Tuliambiwa itajengwa kwa njia nne, sijui hilo litafanyika lini. Tumechoka kuona damu,” amesema Kondo Iddi, mkazi wa Mbagala.

Akizungumza kuhusu foleni, Amina Juma, mkazi wa Kongowe anayefanya shughuli zake Kariakoo, amesema foleni inayoendelea kwenye barabara hiyo inamuathiri kwa kiasi kikubwa kiuchumi.

“Kutoka Kongowe hadi Kariakoo haipaswi kuzidi dakika 30, lakini kwa hii barabara yetu ni kawaida kabisa kutumia saa tatu. Ili uepukane na hilo, inakulazimu kutumia fedha nyingi kutafuta usafiri ambao unaweza kukufikisha kwa haraka, na wakati mwingine njia inafunga hadi pikipiki haiwezi kupita.

“Kuna siku nilitumia saa tatu na nusu kufika Kariakoo na siku hiyo nilikuwa na ahadi na wateja, kutokana na kuchelewa kwangu hawakuweza kunisubiri, nikajikuta nipoteza biashara yangu. Kwa kifupi, Serikali iiangalie hii barabara watumiaji tunateseka,” amesema Amina.

Mariam Suleiman, mama wa watoto watatu wanaosoma, amesema kero hiyo imekuwa ikiathiri hata masomo ya watoto na kuwaweka wazazi kwenye wasiwasi pindi wanapochelewa kurudi nyumbani.

“Wanatoka nyumbani saa 11 alfajiri, lakini bado wanachelewa shuleni. Mwalimu naye haelewi habari za foleni, watoto wanaadhibiwa. Jioni pia ni mtihani, kuna siku mwanangu alirudi saa tatu usiku, ukifuatilia, hakuna tatizo lolote ni foleni ya barabarani,” amesema.

Anord Mndeme, mfanyabiashara wa mbao, amesema ukarabati wa haraka unaweza kuokoa hali hiyo, ikizingatiwa kuwa barabara hiyo ina mchango mkubwa katika uchumi kufuatia uwepo wa viwanda vingi Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.

“Tunaona Serikali ikijenga barabara mpya maeneo mengine, lakini hii ambayo ni ya kibiashara zaidi inasahaulika. Mkuranga kuna viwanda, barabara hii ndiyo inategemewa kusafirisha vinavyozalishwa na kupeleka malighafi. Tunahitaji suluhisho sasa, si kesho,” amesema.

Kwa madereva wa daladala, changamoto ni zaidi ya muda, kwa kile walichoeleza kuwa wanapoteza mafuta mengi kutokana na foleni zisizoisha, na wakati mwingine wanajikuta wakipata ajali.

“Tunapoteza mafuta mengi kwa sababu gari linaendeshwa kwenye gia ndogo muda mrefu. Abiria wanatushushia lawama, lakini ukweli ni kwamba tatizo ni barabara hii.

“Pia, wakati mwingine kwenye foleni kuna hali ya kuchomekeana au kila mmoja kupambana kwa namna yake ili kuwahi kwenye harakati za utafutaji, katika mazingira hayo mnajikuta mnagongana na inakuwa hasara nyingine,” amesema Juma Mrope, dereva wa daladala linalofanya safari kati ya Temeke na Kisemvule.

Agosti 14, 2025, Mwananchi ilizungumza na Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Alinanuswe Kyamba, ambaye ameeleza kuwa ujenzi huo utaanza ndani ya mwezi huu.

Amesema baada ya kusainiwa kwa mkataba, yalikuwa yanafanyika maandalizi ikiwa ni pamoja na kumlipa mkandarasi malipo ya awali, na kinachofuata sasa ni ujenzi unaotarajiwa kuanza ndani ya mwezi huu.

“Kusaini mkataba ni kitu kimoja na kuanza ujenzi ni kitu kingine. Kilichofuata baada ya kusaini ni malipo kwa mkandarasi kwa ajili ya maandalizi ya kazi. Ninachoweza kusema ni kwamba ujenzi wa barabara hiyo utaanza mwezi huu,” amesema.

Kuhusu namna ya kuondoa adha ya foleni kipindi cha ujenzi, amesema miongoni mwa makubaliano katika mkataba ni mkandarasi kuhakikisha magari yanaendelea kupita wakati kazi hiyo inaendelea.

“Watumiaji wa barabara hiyo wasiwe na wasiwasi, ni jukumu la mkandarasi kuhakikisha wakati anafanya kazi yake, magari yanaendelea kupita,” amesema Kyamba.

Wataalamu wamesema kuwa pamoja na upanuzi wa barabara, hatua za kudhibiti msongamano zinahitajika, zikiwemo ujenzi wa njia mbadala, kuhamasisha usafiri wa umma wa uhakika kama BRT, na kuongeza vituo vya mizigo nje ya jiji ili malori makubwa yasiingie katikati ya mji bila sababu.

Wataalamu hao wamebainisha kuwa foleni husababisha miji kupoteza kiasi kikubwa cha fedha, ikiwa ni matokeo ya hasara za moja kwa moja kwa wafanyabiashara wanaochelewesha mizigo na abiria wanaochelewa kazini.

“Hasara hii si ya mtu mmoja mmoja pekee, bali inagusa pato la Taifa. Msongamano unamaanisha muda wa kazi unapotea, gharama za usafirishaji zinaongezeka, na bidhaa zinapoteza ubora sokoni,” amesema mchambuzi wa uchumi, Dk Diana Mwakyusa.

Akizungumzia hilo, mtaalamu wa ujenzi, Mhandisi Ramadhani Lema, amesema ni vyema hatua za haraka zichukuliwe kuipanua barabara hiyo ili kuendana na uhitaji wa sasa.

“Leo tuna magari mara kumi zaidi ya yaliyokuwepo wakati barabara ile inabuniwa. Matengenezo ya vipande hayatasaidia, tunahitaji upanuzi wa kudumu kuwa angalau njia nne, mifereji ya kisasa, taa za barabarani na vivuko salama kwa waenda kwa miguu.

“Tusiangalie kama tu barabara ya Mbagala na Kongowe, bali ni mshipa wa damu wa uchumi wa Taifa. Kila siku inayopotea, tunapoteza mamilioni,” amesema Lema.

Kwa upande wake, mtaalamu wa usafirishaji wa mijini, Hamisi Ndalu, amesema hali hiyo ni matokeo ya kukosekana kwa mipango ya muda mrefu, na kutaleta gharama kubwa zaidi baadaye.

“Hatuwezi kuendeleza miji kwa kasi ya ukuaji wa idadi ya watu bila kuwekeza kwenye miundombinu ya usafiri. Tukichelewa kuchukua hatua, gharama za kurekebisha zitakuwa mara mbili au tatu zaidi ya sasa,” amesema.