Kocha Maximo kutesti mitambo kwa Mabaharia wa KMKM

BAADA ya kambi ya wiki moja kisiwani Zanzibar,  kikosi cha KMC chini ya kocha Mbrazili, Marcio Maximo jioni ya leo Jumapili kinatarajia kujipima nguvu na mabingwa wa Kombe la Shirikisho (ZFF), KMKM kwenye Uwanja wa Mao A uliopo Unguja.

KMC ipo Zanzibar kwa ajili ya kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano ya 2025-2026 tangu wiki iliyopita na leo itatesti mitambo dhidi ya mabahari hao wa kuzuia magendo, KMKM inayojiandaa na michuano ya kimataifa ikiiwakilisha Tanzania michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha wa KMKM, Ame Msimu amesema wameomba kucheza mechi ya kirafiki na KMC  ili kujipima nguvu kabla ya kuingia katika michuano mikubwa huku akikiri kuwa wana kazi ya kufanya.

“Leo jioni tutakuwa na mchezo wa kirafiki na KMC timu ambayo ipo hapa karibu wiki nzima sasa ilifanya mazoezi kujiandaa na Ligi Kuu Bara, nafikiri utakuwa mchezo mzuri kwetu na kwao pia,” amesema Msimu na kuongeza;

“Raha ya maandalizi ni kufanya kwa vitendo tulianza na mazoezi ya kukimbizana kutafuta pumzi, mazoezi ya uwanjani kupigiana mipira sasa tunataka mechi ambayo tayari tumeipata tunacheza na KMC.”

Akizungumzia maandalizi kwa ujumla amesema yanaenda vizuri na mipango yao ni kusuka kikosi shindani ambacho kitafanya vizuri ndani na kimataifa.
Mabingwa hao wa kihistoria wa Zanzibar imepangwa kuvaana na As Port ya Djibouti na ikivuka hapo itaumana na mshindi wa mechi ya Al Merrikh Bentiu ya Sudan Kusini au Azam FC.