BAADA ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Nigeria, timu ya taifa ya Sudan imeonekana kuingia kwenye hali ya kujiamini, lakini kocha Kwesi Appiah ametoa onyo kwa wachezaji wake.
Sudan ipo nafasi ya kwanza katika Gundi D ikiwa na pointi nne, sawa na Senegal iliyopo nafasi ya pili. Kocha Appiah amesema kuwa tofauti ndogo inaweza kuamua nani ataingia hatua ya robo-fainali katika mechi yao ya mwisho ya hatua ya makundi hapo Jumanne dhidi ya Senegal.
“Senegal ni bingwa mtetezi. Hatuna nafasi ya kufanya makosa tunatakiwa kuwa makini,” alisema.
Katika mechi mbili za awali, Sudan imeonyesha kiwango kizuri kwenye kujilinda, timu hiyo imeruhusu bao moja tu, lililofungwa na Congo katika mechi ya kwanza iliyomalizika kwa sare ya 1-1.
“Ukuta wetu umeimarika, lakini hatuwezi kuridhika na hali hii,” alisema Appiah.
Senegal, kwa upande wake, ilianza mashindano kwa kuichapa Nigeria bao 1-0, kisha kutoa sare dhidi ya Congo.