Mabaki ya mifugo iliyochinjwa yanavyogeuka kitoweo Dar

Dar es Salaam. Katika jiji la kibiashara la Dar es Salaam, karibu kila sehemu ya kuku, mbuzi au ng’ombe sasa imekuwa fursa ya biashara na mlo.

Kuanzia miguu, utumbo, vichwa, ashua, matiti ya ng’ombe, kongosho na hata ngozi, sehemu za mifugo ambazo zamani zilikuwa zikitupwa, sasa zinauzwa kwa wingi kwenye vibanda vya barabarani, hasa katika vituo vya mabasi nyakati za jioni.

Mara nyingi hupikwa kwa kuchomwa au kuchemshwa, na hutolewa pamoja na ndizi za kuchoma na kachumbari na pilipili inayotengenezwa kwa nyanya, vitunguu na limao.

Uchunguzi wa Mwananchi  uliofanyika mwishoni mwa wiki umebaini kuwa wakazi wa maeneo ya kipato cha chini, ambao hawawezi kumudu vipande bora vya kuku, mbuzi au nyama ya ng’ombe, wamegeukia sehemu hizi kama mbadala wa bei nafuu kwa nyama ya kawaida.

Mkazi wa Buguruni, Ibrahim Juma, amesema hununua viungo hivyo kwa takriban Sh3,000, kiasi cha kutosha kwa mlo wa ugali au wali.

“Vinasaidia watu wenye kipato kidogo kufurahia kile tunachoweza kupata kutoka kwenye kuku, mbuzi na ng’ombe. Hii ni kawaida kwa familia nyingi katika mtaa wangu,” amesema.

Juma anapenda zaidi korodani za mbuzi kwa ladha yake, lakini huepuka kupeleka nyumbani. “Si utamaduni wetu wa Kiafrika kutaja wazi sehemu za siri za wanyama. “Nazila kwenye kibanda na kubeba viungo vingine nyumbani kwa ajili ya familia yangu,” amesema.

Virutubisho, hatari za kiafya

Ofisa Utafiti Mwandamizi wa Masuala ya Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), Maria Ngilisho, amesema vyakula hivyo vina virutubisho na havina madhara kama vitapikwa kwa usafi na kwa ukamilifu.

“Kula sehemu za wanyama kama miguu ya kuku na utumbo ni chanzo nafuu cha protini, kolajeni na virutubisho vingine muhimu kama madini na vitamini kwa kaya nyingi za kipato cha chini na cha kati,” amesema.

Amesema sehemu zilizo na kolajeni kwa wingi kama miguu ya kuku na ngozi za wanyama (ng’ombe, kuku na mbuzi miongoni mwa wengine) zinathaminiwa kwa kuimarisha afya ya viungo na kuboresha unyumbufu wa ngozi.

“Mkia wa ng’ombe hutoa protini ya ubora wa juu na ladha tamu katika supu na mchuzi,” ameongeza mtaalamu huyo wa lishe.

Kuhusu madai kuwa kula korodani huongeza uwezo wa tendo la ndoa kwa wanaume, Ngilisho amesema hizo ni imani potofu, akieleza kuwa uwezo wa tendo la ndoa unategemea mambo mengi kama ulaji bora, mtindo wa maisha na kutokuwa na msongo wa mawazo.

“Kwa afya, wataalamu wanashauri kila kitu kifanywe kwa kiasi, kula kwa kiasi, fanya mazoezi kwa kiasi. Andaa chakula kwa njia ya usafi ili kuhakikisha vyakula hivi vya asili vinabaki salama na vyenye manufaa… Hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha imani hizo,” amesema.

Ameongeza kuwa ni muhimu kusafisha vizuri hasa utumbo ili kuepuka maambukizi ya bakteria, na ameonya kuwa kutumia viungo vingi au kukaanga sana kunaweza kupunguza thamani ya virutubisho. Pia, kula vyakula vya kukaanga kupita kiasi kunaweza kusababisha athari kiafya.

Katika kituo cha mabasi cha Segerea, Fredy Shirima amekuwa akiuza bidhaa hizi kwa miaka mitatu, akiihudumia familia yake ya watu watano.

Hupata miguu ya kuku, utumbo na vichwa kutoka masoko ya Buguruni na Temeke, na hupata ashua za mbuzi, matiti, kongosho na ngozi kutoka kwa wasambazaji watatu.

“Nawalipa wanaoniletea hizi nyama siku moja kabla na wanatuma waendesha bodaboda kwenda kuchukua viungo hivyo. Kwa siku nzuri, naingiza hadi Sh200,000; siku za kawaida naingiza Sh150,000,” amesema.

Shirima amekiri kuwapo kwa imani potofu kuhusu baadhi ya viungo, kama vile ashua za mbuzi kuhusishwa na ongezeko la nguvu za kiume hasa kwa wanaume.