Peshawar. Zaidi ya watu 300 wamefariki dunia nchini Pakistan kufuatia mafuriko makubwa yaliyokumba maeneo mbalimbali kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Mafuriko hayo yamesababishwa na mvua kubwa iliyonyesha kwa siku mbili mfululizo katika maeneo ya milimani ya jimbo la Khyber Pakhtunkhwa, na kusababisha vifo vingi pamoja na uharibifu mkubwa wa mali za watu.
Kwa mujibu wa ripoti ya tovuti ya habari ya Reuters, mamlaka za kudhibiti maafa nchini Pakistan zimesema kuwa hadi asubuhi ya leo Jumapili ya Agosti 17, 2025 watu 307 wamethibitishwa kufariki dunia, huku wengine wengi wakiwa bado hawajulikani walipo.
Shughuli za uokoaji zinaendelea kwa dharura katika maeneo yaliyoathirika.
Msemaji wa huduma rasmi ya uokoaji, Bilal Faizi, ameeleza kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka zaidi kadri wanavyoendelea na shughuli za kuokoa watu walioko chini ya vifusi vya nyumba zilizoporomoka.
Wilaya ya Buner, iliyoko kaskazini mwa mji mkuu Islamabad, imekuwa eneo lililoathirika zaidi ambapo vifo 184 vimeripotiwa hadi sasa.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje, Ishaq Dar, amesema vikosi vya kiraia na jeshi vinaendelea na shughuli za uokoaji na misaada, huku Waziri Mkuu akiita kikao cha dharura.
Katibu Mkuu wa Mkoa, Shahab Ali Shah, amesema maofisa wa Serikali wametumwa maeneo yaliyokumbwa na mafuriko kusimamia shughuli za misaada na kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea.
Aliongeza kuwa kambi za matibabu zinaandaliwa kwa waathirika wa mafuriko pamoja na mpango wa kugawa chakula kwa familia zilizopoteza makazi.