……………
Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan katika Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi
Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) uliyofanyika katika
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Ivato, Antananarivo nchini Madagascar.
Katika Mkutano huo Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa
amekabidhi Uenyekiti wa SADC kwa Rais wa Jamhuri ya Madagascar Mhe. Andry
Nirina Rajoelina utakaodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja. Vilevile Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imekabidhi uenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama
(SADC Organ Troika) kwa Jamhuri ya Malawi mara baada ya kuhitimisha uongozi wa
mwaka mmoja wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ulioanza Agosti 2024.
Akisoma hotuba ya ufunguzi Mwenyekiti wa SADC anayemaliza muda wake,
Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa pamoja na mambo mengine amempongeza
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa
kuiongoza vema Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama na kuhakikisha amani na
utulivu katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini Mwa Afrika.
Mkutano huo umejadili hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa Mpango
Mkakati Elekezi wa kanda, kuanisha mafanikio na changamoto za utekelezaji.
Utekelezaji umejikita katika nguzo kuu nne zikiongozwa na nguzo kuu ya Amani,
Usalama na Utawala wa Kidemokrasia. Nguzo nyingine ni maendeleo ya viwanda na
utangamano wa masoko, Maendeleo ya miundombinu katika kuchagiza utangamano
pamoja na maendeleo ya kijamii na rasilimali watu.
Miongoni mwa mafanikio yaliyojadiliwa ambayo yamepatikana ni pamoja na
kupungua kwa matukio ya ugaidi, kuimarika kwa demokrasia katika Kanda kupitia
chaguzi huru na haki, kuongezeka kwa huduma za kifedha, kuongezeka kwa thamani
ya mauzo ya bidhaa za viwanda na kuongezeka kwa miamala iliyofanyika kupitia
mfumo wa malipo wa kikanda (Real Time Gross Settlement – RTGS).
Katika Mkutano huo washindi mbalimbali wa Tuzo zinazotolewa na SADC
wametangazwa ikiwemo Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari kutoka nchini Tanzania
Crispin Kamugisha aliyetangazwa mshindi katika uandishi wa insha na kuzawadiwa
dola elfu moja mia tano.
Kauli mbiu ya Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Wanachama
wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ni “Kuendeleza Viwanda, Mageuzi ya Kilimo na Matumizi bora ya Nishati kwa
ustahimilivu wa kanda ya SADC” (Advancing
Industrialisation, Agricultural Transformation, and Energy Transition for a
Resilient SADC).