DAKIKA 120 zimetosha kwa kocha mpya wa KMC, Mbrazili Marcio Maximo kupima kikosi chake baada ya mazoezi ya wiki mbili kwa kulazimishwa sare ya 1-1 na maafande wa KMKM, lakini akiwa na kazi kubwa ya kufanya kwa safu ya ushambuliaji ya timu hiyo.
Timu hizo imecheza dakika 120 zote zikibadili wachezaji kwa ajili ya kutoa nafasi kwa kila mchezaji na kupata nafasi ya kucheza na kumaliza bila mbabe.
KMC ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 105 kupitia kwa mshambuliaji Akram Mhina Omary ‘Haaland’.
Mchezo huo ulioanza saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Mao, mjini Unguja, ubora wa KMKM katika maeneo yote kiungo, winga na mabeki umeifanya KMC ishindwe kuona lango lao mapema dakika za jioni ndio walipata bao hilo.
Licha ya KMC kuongoza kwa bao moja ilionekana kuhitaji bao lingine zaidi lakini uimara wa safu ya ulinzi ya KMKM uliwazuia kupata bao lingine na kujikuta timu zote zinamaliza dakika 120 kwa sare ya bao 1-1.
Mukrim Hassan ndiye aliyeisawazishia KMKM kwa mpira wa kichwa.
Kwa dakika 90 za awali timu zote zilionyesha ufundi hasa eneo la kiungo na kuwapa burudani mashabiki waliohudhuria.l
Kikosi cha KMKM kimeonyesha mchezo mzuri kikiwapa kipimo sahihi KMC pamoja na wao kujifua kwa mchezo wao wa Kombe la Shirikisho dhidi ya AS Port.