Morocco yaifuata Taifa Stars Kwa Mkapa

USHINDI wa mabao 3-1 iliyopata Morocco mbele ya DR Congo, imewafanya mabingwa hao mara mbili wa michuano ya CHAN kufunga safari kuifuata Tanzania katika mechi ya robo fainali ya michuano ya msimu huu inayofanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.

Wenyeji wa Kundi A, Kenya yenyewe imesalia jijini Nairobi baada ya kuongoza msimamo kutokana na ushindi wa bao 1-0 iliyopata katika mechi ya mwisho dhidi ya Zambia iliyomaliza michuano bila ushindi wala pointi yoyote ikiwa ni rekodi kwa taifa hilo kutoka Kusini mwa Afrika.

Morocco imemaliza kama mshindi wa pili wa kundi hilo na sasa itavaana na Tanzania wikiendi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, wakati Kenya itakwaruzana na Madagascar iliyoshika nafasi ya pili katika Kundi B lililocheza mechi zao hapa Tanzania.

Mabao mawili kutoka na Oussama Lamlioui katika kila kipindi na jingine la Mohamed Hrimat       kwenye Uwanja wa Nyayo, jijini Nairobi yalitosha kuifungisha virago DR Congo, mabingwa mara mbili ikilingana na Morocco, licha ya Japhte Kitambala kufunga bao la kufutia machozi la DR Congo.

Lamlioui anayekipigia RS Berkane ambao ni mabingwa wa Kombe la Shirikisho msimu uliopita sasa ndiye kinara wa mabao katika CHAN 2024 akifikisha matatu, huku Kitambala na Hrimat kila mmoja akiwa na mawili kama Ryan Ogam wa Kenya aliyefunga bao pekee dhidi ya Zambia.

Katika mechi hiyo ya wenyeji iliyopigwa kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, jijini Nairobi Ogam alifunga bao hilo muhimu dakika ya 75 akimalizia pasi ya Boniface Muchiri na kuifanya Kenya inayonolewa na Benni McCarthy kumaliza kibabe katika kundi hilo ikivuna pointi 10.

Kwa sasa kocha huyo, ana kibarua cha kukabiliana na Hemed Morocco wa Tanzania aliyeiwezesha pia Tanzania kuandika rekodi ya kushinda mechi tatu mfululizo za hatua ya makundi ya michuano ya CAF sambamba na kumaliza hatua ya makundi Strs ikikusanya pia pointi 10 kama Kenya.

Mapema leo kocha Morocco, alisema mechi ya jana usiku dhidi ya Afrika ya Kati iliyoisha kwa suluhu ilikuwa ni kama darasa kwa wachezaji wa kikosi hicho, akibainisha wamepata somo ambalo anaamini litawasaidia katika maandalizi ya mechi ya robo fainali ya mashindano ya CHAN 2024.

Kocha huyo alisema ameshazungumza na wachezaji ili kuhakikisha wanajipanga na kutumia kila nafasio katika mechi ijayo itakayopigwa Jumamosi usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ili kuandika historia nyingine ya kutinga nusu fainali ya michuano hiyo ya nane tangu ilipoasisiwa 2009.