Ramadhan Kapera, Polisi Tanzania kuna jambo

POLISI Tanzania imeanza mazungumzo ya kumrejesha aliyekuwa mshambuliaji wa kikosi hicho, Ramadhan Kapera baada ya nyota huyo kumaliza mkataba wake na TMA ya Arusha, huku kukiwa hakuna mazungumzo ya kuongeza mpya.

Mchezaji huyo aliyetamba na timu za Mbeya Kwanza, Geita Gold, KMC na Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars inaelezwa ni pendekezo la kocha wa Polisi Tanzania, Mbwana Makata anayemtaka ili kuboresha eneo la ushambuliaji.

Makata amejiunga na Polisi akirithi mikoba ya Mussa Rashid aliyetokea Biashara United aliyeiongoza msimu uliopita katika Ligi ya Championship na kumaliza nafasi ya 10 ikiwa na pointi 33 baada ya kushinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13 kati ya 30.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kapera alisema kwa sasa ni mchezaji huru na nafasi ya kucheza tena TMA msimu ujao ni ndogo, ingawa hajafanya uamuzi wa mwisho wa timu atakayoichezea kwa sababu zipo ofa mbalimbali ambazo anaendelea kuzifanyia kazi.

“Nimeachana vizuri na TMA baada ya mkataba wangu kuisha. Mazungumzo ya kuongeza mwingine mpya yapo kwa sababu ni kweli bado wanahitaji huduma yangu japo ni ngumu kuendelea kuichezea tena, hivyo naangalia fursa nyingine,” alisema Kapera.

Msimu wa 2024-2025 Kapera aliifungia TMA mabao sita katika Ligi ya Championship huku akiiwezesha kumaliza nafasi ya tano na pointi zake 53 baada ya kushinda mechi 15, sare nane na kupoteza saba ikifunga mabao 40 na kuruhusu 29.

Polisi Tanzania inapambana ili kurejea Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja 2022-2023 ilipomaliza nafasi ya 15 na pointi 25 kufuatia kushinda mechi sita, sare saba na kupoteza 17 ikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.