Ramli chonganishi yadaiwa kusababisha mauaji ya mwananfuzi wa sekondari Babati

Babati. Mwanafunzi wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Qash iliyopo wilayani Babati, mkoani Manyara, Yohana Konki (17) anadaiwa kuuawa na wanafunzi wenzake kwa madai ya wizi wa kishkwambi.

Kufuatia tukio hilo,  wanafunzi 11,  msimamizi na mlinzi wa shule hiyo wanashikiliwa kwa uchunguzi wa kifo hicho.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara,  Ahmed Makarani akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Agosti, 17, 2025 amesema tukio hilo limetokea saa 10 alfajiri ya Agosti 16 shuleni hapo.

Kamanda Makarani amedai kuwa chanzo cha kifo cha mwanafunzi huyo ni baadhi ya wenzake kumpiga kwa kumtuhumu ameiba simu aina ya tablet.

Amesema baada ya mmoja kati ya wanafunzi wa shule hiyo kupoteza simu alikwenda na wenzake kwa mganga wa kienyeji na kupiga ramli chonganishi ili kumbaini mwizi.

“Walipotoka huko walimfuata huyo mwanafunzi na kumtuhumu wizi kisha wakamlazimisha awarudishie na alipokataa kuwa hakuiba walimpiga na kusababisha kifo chake,” amedai Kamanda Makarani.

Amesema wanawashikilia wanafunzi 11 kwa uchunguzi wa kifo hicho pia wamewakamata msimamizi na mlinzi wa shule kwa mahojiano ya tukio hilo.

Ametoa wito kwa uongozi wa shule hiyo kuweka kamera ili kuepuka matukio kama hayo kwani wanafunzi hao wangeweza kumbaini mwizi kuliko kutegemea ramli chonganishi.

“Tunalaani mno tukio hilo ila kungekuwa na CCTV kamera hapo kungeweza kuwasaidia na wanafunzi hao wangembaini mwizi wao kuliko kwenda kupiga ramli chonganishi,” amesema Kamanda Makarani. 

Ofisa Tarafa wa Babati mkoani Manyara, Msalla Msalla akizungumza na wakazi wa kata ya Qash baada ya kutokea mauaji ya mwanafunzi anayedaiwa kuuawa na wenzake kwa wizi wa simu. Picha na Joseph Lyimo

Ofisa tarafa ya Babati, Msalla Msalla amesema kuwa wanafunzi hao hawakuwa na uthibitisho wowote wa kumuhukumu mwanafunzi mwenzao kisa wanadai ameiba simu aina ya tablet.

Amesema wanafunzi hao walipaswa kufikisha taarifa za wizi kwa walimu kuliko kwenda kwa mganga wa kienyeji na kuchukua hatua ya kumpiga mwenzao kwa jambo ambalo halina ushahidi.

“Pia tumeagiza msimamizi wa wanafunzi na mlinzi wa shule wakamatwe ili kufanyiwa mahojiano na kubaini walikuwa wapi mwanafunzi akipigwa hadi anafariki,” amesema Msalla.

Amewatoa hofu wakazi wa eneo hilo na kuacha kusababisha taharuki kwani Serikali imeshachukua hatua kwa kuwakamata wahusika wanaohisiwa kufanya tukio hilo.

Shangazi wa marehemu (Yohana Konki), Elizabeth Konki amesikitishwa na tukio hilo kwani wamekatisha ndoto za kijana wake ambaye ameuawa kifo asichostahili.

Amesema endapo mwanafunzi huyo angekuwa amefanya tukio la wizi wasingepaswa kumpiga na kumuua zaidi ya kufikisha hilo kwa walimu wao.

Mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Hassan Juma amedai kuwa wanafunzi hao walimpiga mwenzao kwa kumshambulia kwa fimbo sehemu mbalimbali kutokana na majibu ya mganga wa kienyeji.

“Walipotoka kwa huyo ustadhi na kupewa majibu kuwa Konki ndiye amechukua hiyo simu, walimuuliza na alipokataa kuwa hakuchukua walimpiga sehemu mbalimbali,” amedai.

Amedai baada ya kupigwa sana na kuumizwa aliwaeleza kwamba simu hiyo alimpa dada yake na alipowapa namba waliipiga ila haikupatikana.