Unguja. Katika kuleta mageuzi mapya ya ujumuishaji, usawa na haki kwa watu wenye ulemavu Tanzania, unatarajiwa kuzinduliwa mradi wenye thamani ya Sh20 bilioni.
Mradi huo wa miaka mitano unalenga kufanya kazi katika maeneo makuu matano ambayo ni utetezi wa haki za watu wenye ulemavu, elimu jumuishi, uwezeshaji kiuchumi na afya jumuishi utakaozinduliwa Agosti 20, 2025 na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud.
Hayo yamesemwa leo Agosti 17,2025 na Mkurugenzi mkaazi wa Shirika la Watu Wenye Ulemavu Norway (NAD), Abdulla Amair alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Unguja kuhusu uzinduzi wa mradi huo. Ambapo amesema unalenga kuongeza mwamko wa watu na taasisi katika kuzitambua na kuzifanyia kazi haki za watu wenye ulemavu ili kuondoa vikwazo.
Katika suala la utetezi wa haki, zitajengewa uwezo jumuiya za watu wenye ulemavu ili wazitambue haki zao na kuzitetea zikiwemo taasisi binafsi na Serikali ili zishiriki katika utetezi huo, ambapo taasisi 18 za watu wenye ulemavu zinatarajiwa kujengewa uwezo.
“Katika eneo la elimu mjumuishi ni kufanya kazi na watu wenye ulemavu na wizara za elimu katika kutengeneza kukuza ustawi wa elimu mjumuisho, ili kuwe na mfumo kwa wote na watu wenye ulemavu wawe na uwezo kusoma na wenzao darasani,” amesema.
Mradi huo wa CADiR (Collective Actions for Disability Right) ni mpango wa miaka mitano utakaotekelezwa kwa Zanzibar na Tanzania bara kuanzia mwaka 2025 hadi 2029, ukifadhiliwa na Shirika la Norwegian Agency for Development (Norad) la nchini Norway kwa ushirikiano na mashirika tofauti ya Norway na Tanzania na Serikali zote mbili za Muungano.
Amesema zitafikiwa shule 110 ambapo walimu watajengewa uwezo na jamii inayozunguka shule hizo baada ya miaka mitano elimu hiyo itakuwa imekuwa.
Kwa upande wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, mradi huo unatarajia kufika shehia nne kwenye wilaya zote 11 na watafungua vikundi vitano vya kuweka na kukopa vyenye watu wenye ulemavu, ambapo baada ya miaka mitano watakuwa na vikundi vyenye watu wasiopungua 220.
“Kwa hiyo watu wenye ulemavu 660 watafaidika kwenye eneo la uwezeshaji kiuchumi, watafaidika kwa mikopo kwa mafunzo ya kufanya biashara na kutengeneza mazingira waweze kuajirika,” amesema.
Pamoja na mambo yote hayo pia kutakuwa na mazingira ya upatikanaji wa vifaa saidizi kwa walemavu wasiopungua 475 sambamba na kufanya uchunguzi wa afya kwa watu 4,300 kwa walemavu na kutoa matibabu ambapo miongoni mwao watu 700 watafanyiwa upasuaji wa macho.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Zanzibar, Ussi Khamis Debe amesema licha ya hatua kubwa zilizopigwa bado kuna changamoto kubwa katika kuhakikisha usawa na fursa kwa watu wenye ulemavu.
“Uzoefu unaonyesha watu wenye ulemavu wanakosa huduma bora kutokana na miundombinu, upungufu wa vifaa saidizi, na uhaba wa wataalamu wa lugha ya alama huku sekta ya ajira ikikabiliwa na mitazamo hasi, kwa hiyo kuja kwa mradi huu utaweza kusaidia kuondoa vikwazo hivyo,” amesema Ussi.
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Jumuiya ya Watu wenye ulemavu Zanzibar (Shijiwaza), Mwandawa Khamis Mohammed amesema utakuwa kwa masilahi ya walemavu, hivyo akawataka kushiriki katika shughuli zao wasiwe nyuma ili kujiletea maendeleo yao binafsi na Taifa.
Kati ya fedha hizo za mradi, Zanzibar itapata Sh17.8 bilioni sawa na asilimia 76 ya fedha zote.