Shughuli pevu madereva wasiosoma kupata, kuhuisha leseni hakuna tena njia za panya

Dar es Salaam. Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Kipolisi Kawe, Rose Maira amepigilia msumari suala la madereva wasiosomea taaluma hiyo kutohuisha au kupata leseni kutokana na taratibu na sheria za sasa kuwabana.

Amesema utaratibu uliopo sasa uliotokana na maboresho ya Jeshi la Polisi upande wa usalama barabarani pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuimarisha usimamizi9 katika eneo hilo,  kwa kuwa awali ilionekana madereva hawapiti vyuoni wanajifunza mitaani hali inayosababisha ajali nyingi.

Ameyasema hayo katika hafla ya mahafali ya wahitimu 160 wa mafunzo ya udereva katika Chuo cha udereva Mlimani yaliyofanyika Tegeta jijini Dar es Salaam.

“Sasa kinachotakiwa ni cheti cha udereva cha chuo kinachotambuliwa na Serikali chenye namba ya usajili na tunataka intake yako kwa sababu tutakuuliza kuhakiki ndipo unaanza utaratibu wa leseni,” amesema.

“Mwisho wao umefika kwani kwa sasa hakuna kupata leseni bila ya kusoma tunaingia chuo ulichosoma hakuna kupitia njia za mkato tena, wewe ni mtoto wa nani hicho kitu hakipo,” amesisitiza.

Akizungumza na Mwananchi, Balozi wa Usalama Barabarani kutoka Asasi ya RSA Tanzania, Ramadhan Msangi amesema jambo hilo linapaswa kupongezwa kwa sababu mwanzo kulikuwa na malalamiko ya madereva kutokuwa na elimu.

“La msingi, namna gani tunaboresha mitaala iendane na hali halisi ya mazingira ya sasa kuwe na vitu vya msingi ambavyo dereva anapaswa kujua,” amesisitiza Msangi.

Akitoa elimu ambayo huwezi kuipata mtaani Maira amesema mfano dereva akikutwa hana leseni pengine ameisahau nyumbani wakati anaendesha gari hapaswi kutozwa faini, bali anayo nafasi ya kisheria kupeleka leseni hiyo ndani ya saa 72.

“Sheria ya usalama barabarani inamtaka dereva awe na leseni halisi muda wote iendane na chombo anachoendesha kwa wakati husika. Lakini unapokamatwa unaambiwa unaandikiwa faini kavu.

“Lakini tuna uhakika una leseni na unatuonesha kwenye simu unayo ila umeisahau na unaambiwa unaandikiwa kwa kuwa hujatembea na leseni halisi, kumbe hapana haki na wajibu wa dereva sheria imempa siku tatu kuleta leseni hiyo kabla askari hajachukua uamuzi,” amesema.

Amesema ukileta leseni ndani ya muda huo hutakuwa na kosa la kuendesha bila ya kuwa na leseni. Amesema madereva wakienda shule watafahamu hayo yote sambamba sheria za usalama barabarani hali itakayomaliza ajali.

Akizungumza na uongozi wa shule hiyo amesisitiza kuwapa nafasi ya kuendelea kusoma wanafunzi ambao hawajaelewa.

“Kuliko kuwa na gari ulilobandika alama ya L nyekundu (kwa wale wanaojifunza) kwani ni kosa la kisheria kwa sababu alama hiyo inapaswa kuwekwa na mwanafunzi anayefundishwa na mwalimu mwenye cheti cha ualimu wa udereva sio mtu yeyote tu anayekufundisha,” amesisitiza.

Mmoja wa  wahitimu wa chuo hicho,  Hadija Mkwizu amesema madereva wasiosoma wanaweza kuwa chanzo cha ajali kwa kuwa  hawana elimu hivyo wanapaswa wakasome.

Noel Steven amesema sheria za barabarani ni jambo la muhimu kujifunza ili kupunguza ajali hivyo ambao hawajasoma hawana budi kufanya hivyo.

Mkurugenzi wa chuo hicho, Cafti Kimaro amesema baadhi ya watu kupanda kupita njia zisizo rasmi wanapaswa kuachana nazo kuepusha ajali zisizo na sababu.