Taharuki jeneza linalodaiwa kufukuliwa kaburini likitelekezwa bila maiti

Shinyanga. Jeneza lenye mabaki ya sanda bila maiti limekutwa limetelekezwa kando ya barabara, eneo la korongo linalopitisha maji wakati wa mvua, na kuzua taharuki miongoni mwa wakazi wa Manispaa ya Kahama.

Kwa mujibu wa mashuhuda, jeneza hilo lilikutwa Mtaa wa Nzengo ya Izuga, Kata ya Mhongolo, na tangu kugundulika kwake limeibua hofu na maswali mengi miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, huku baadhi wakilitafsiri kama tukio lenye uhusiano na imani za kishirikina.

Tukio hili limetokea katika kipindi ambacho Taifa linaelekea kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, jambo linaloongeza hofu na hisia mbalimbali za kisiasa miongoni mwa wananchi.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mhongolo, Emanuel Nangale, amethibitisha kutelekezwa kwa jeneza hilo na kusema lina dalili kuwa limefukuliwa kaburini.

“Ni kweli jeneza hilo tumeliona na kwa muonekano wake, halina shaka kwamba limeshatumika. Lilikuwa na kamba, udongo na hata alama za damu ndani. Kwa vyovyote vile, lilikuwa na mwili wa binadamu kabla ya kufukuliwa,” amesema.

Amesema walibaini uwepo wa jeneza hilo kwenye moja ya shimo lililopo pembezoni mwa barabara jirani na makazi ya watu eneo hilo Agosti 12, 2025, na baadaye walitoa taarifa kwa polisi ambao walifika na kulichukua.

Mpaka sasa, haijafahamika nani aliyehusika na sababu kamili ya kutelekeza jeneza hilo katika eneo la makazi ya watu.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga, Kennedy Mgani, amesema hana taarifa za tukio hilo na kueleza kuwa analifuatilia, litakapokamilika atalitolea ufafanuzi.

Hata hivyo, baadhi ya mashuhuda waliofika eneo hilo wamedai kuwa jeneza hilo lilionekana kuwa lilishatumika, likiwa na kamba za kushushia kaburini, mavumbi, udongo, nguo, sanda, na hata harufu kali iliyodhaniwa kuwa ya mwili uliokuwa ndani.

“Nililiona kwa macho yangu. Lilikuwa na vumbi, kamba, na harufu kali. Linaonekana kama lilifukuliwa kutoka kaburini. Sidhani kama hili ni jambo la kawaida. Ukizingatia kipindi hiki cha kisiasa, si ajabu tukio hili likawa na uhusiano na imani za kishirikina,” amesema Said Sharifu, mkazi wa Izuga.

Naye Khadija Salum, mkazi mwingine wa eneo hilo, ameeleza kuwa tukio hilo liliwafanya baadhi ya wananchi waende kukagua makaburi ya jamaa zao ili kujiridhisha kuwa hayakufukuliwa.

“Tulikuwa na hofu kubwa. Hata makaburi mapya tuliyakagua, lakini tulibaini kuwa yote yako salama. Wapo waliolihusisha tukio hili na wagombea wanaotafuta madaraka kwa njia za kishirikina,” amesema Khadija.

Sarafina Boniface naye amesimulia jinsi walivyogundua jeneza hilo baada ya watu kukimbilia eneo hilo kwa mshangao.

“Baada ya kufika, tulikuta jeneza kwenye shimo, jirani kabisa na makazi yetu. Tulimuita trafiki wa jirani aliyesaidia kuligeuza na kugundua harufu na nguo zilizokuwemo ndani,” amesema.