Dar es Salaam. Matumizi hasi ya akili unde (AI), mashambulizi ya kimtandao, usalama pamoja na ujenzi wa uchumi wa kidijitali ni miongoni mwa mambo yaliyoing’ata sikio Serikali kupitia Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), kuwanoa wataalamu wa Kitanzania katika sekta hiyo.
Katika zama hizi za teknolojia hasa ya akili unde, kumekuwa na matumizi hasi yanayotokana na programu kama Deepfake zinazotengeneza maudhui ya uongo, mashambulizi ya kimtandao, udukuzi wa mifumo suala linalohitaji wataalamu wa ulinzi wa mitandao wenye ujuzi.
Akizungumza kwenye ufungaji wa mafunzo ya usalama wa mtandao yaliyoandaliwa na Tume ya Tehama kwa kushirikiana na Wakala wa Usalama wa Mtandao Korea Kusini (KISA), Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Dk Nkundwe Mwasaga amesema mafunzo hayo kwa wataalamu yamewaongezea ujuzi muhimu unaohitajika kwenye dunia ya sasa.

“Eneo la usalama wa mtandao ni pana, mafunzo waliyopata yanahusu kufanya uchunguzi wa taarifa za kidijitali. Upotoshaji namna ya kujua maudhui kama ni kweli au si kweli. Wataalamu wamepata ujuzi mpya katika eneo zima la usalama wa mtandao,” amesema Dk Mwasaga.
Amesema nchi ya Korea Kusini imedhamiria kuwa na wataalamu wa usalama wa mtandao wapatao 10,000 wenye uwezo wa ulinzi wa mitandao ya kidijitali, huku Tanzania ikinuia kuwapata zaidi ya hao kwa kuwa watumiaji nchini ni wengi hasa katika uchumi wa kidijitali.

“Uchumi wetu ni mkubwa tunahitaji kuwa na wataalamu wengi kila wilaya na tarafa wawalinde na kuwafundisha Watanzania,’ amebainisha huku akiahidi kufanya mafunzo mengi zaidi.
Amesema Tume hiyo inajenga uchumi wa kidijitali kuwa salama ili kuongeza imani ya watumiaji ndio maana wanawapa mafunzo wataalamu wa eneo hilo.
Akizungumza baada ya kupata mafunzo hayo, Msimamizi wa bidhaa za online kutoka Mwananchi Communications Limited (MCL), Frank Galos amesema kwa upande wa vyombo vya habari vinapaswa kuwa na vitengo vya uchunguzi mtandaoni vyenye watu wabobezi eneo la udukuzi.
“Lazima kuwe na wataalamu wa kugundua mtu anadukuliwaje, pia wenye kujua kutafuta ushahidi wa makosa ya kimtandao, tunawezaje kurudisha faili lililofutika au kudukuliwa, vitu vyote hivyo lazima vijitosheleze,” amesema.
Ofisa Ulinzi wa Taarifa binafsi kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Lilian Chambiri amesema mafunzo hayo yameongeza ujuzi katika kutafiti matukio mbalimbali yanayotokea ikiwamo taarifa hasi za watu zilizosambazwa ili kubaini chanzo.

Mtaalamu wa usalama mtandaoni kutoka CRDB, David Kway amesema mafunzo yamehusu uchunguzi ili kujua wahusika na mtandao mzima wanaotekeleza matukio ya kimtandao. Lengo ni kusaidia kupambana na uhalifu kidunia.
“Mfano katika taasisi za kifedha kuna mashambulizi ya kiteknolojia benki zinawindwa hadi na watu wa nje ya mabara. Lazima tuendelee kujifunza vitu kama hivi,”ameshauri.
Katibu Mtendaji Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Dk Goodwill Wanga amesema kuna umuhimu wa kuongeza wataalamu na mafunzo ya uchunguzi wa mifumo ya kidijiti kutokana na uwepo wa ujenzi wa uchumi wa kidijitali.
“Katika uchumi wa kidijitali taarifa ikiwemo za kibiashara lazima tuhakikishe zinakuwa salama. Tumeimarishwa kwenye mbinu za kujua aina ya makosa, chanzo, nani amehusika, wakati gani na wametumia mifumo gani, na sisi tumejua kuhakikisha mifumo yetu kuwa salama,” amesema Dk Wanga.