Kamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Mhe. Awadh Ali Said, akizungumza wakati wa kufunga mafunzo.
Wasimamizi wasaidizi wa majimbo ya uchaguzi Zanzibar wakila kiapo maalum cha utekelezaji wa majukumu yao hafla iliyofanyika katika ukumbi wa jaji mstaafu Hamid Mahmoud makao Makuu ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC Maisara picha na Nihifadhi Abdulla
TUME ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imehitimisha mafunzo ya siku tano kwa wasaidizi wa wasimamizi wa majimbo ya uchaguzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo washiriki wametakiwa kutumia mafunzo hayo kwa ufanisi ili kuhakikisha zoezi linafanyika kwa haki na amani.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Kamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Mhe. Awadh Ali Said, amesema mafunzo yamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na utayari wa washiriki pamoja na ufanisi wa uwasilishaji mada. “Nimepata taarifa kuwa mafunzo haya yamekwenda vizuri kwa sababu kuu mbili, kwanza washiriki walikuwa tayari kupokea masomo, na pili majadiliano yalivyokuwa yakiendeshwa imeonyesha mko tayari kulitekeleza jukumu hili kwa mustakbali wa demokrasia ya nchi yetu,” amesema.
Kamishna Awadh amesema mada zilizojadiliwa zitaleta mchango mkubwa kwa watendaji wa muda ambao watasimamia vituo vya kupigia kura, hivyo washiriki wa mafunzo wanapaswa kuyatendea haki kwa kuyafikisha kwa ufanisi. “Niwaombe sana maafisa mliopata mafunzo haya kwamba mkayatendee haki kwa watendaji wa muda kwani mtakapoyatoa kikamilifu kazi ya kuendesha Uchaguzi Mkuu itakuwa na ufanisi mkubwa na matokeo chanya,” ameongeza.
Aidha, amewakumbusha wasaidizi hao kuwa nafasi zao ni kiunganishi muhimu kati ya wapiga kura na Tume, hivyo ni lazima watoe huduma bila upendeleo wowote. “ niwaasa wasimamizi wasaidizi wa majimbo yote kwamba katika kutekeleza majukumu yenu mwende mkatende haki, kila mwenye haki ya kupiga kura aitekeleze bila kikwazo,” amesisitiza.
Ameonya pia dhidi ya mihemko ya kisiasa na mapendeleo, akisema kufanya hivyo ni sawa na kukiuka sheria na maadili ya kazi. Kamishna huyo ameongeza kuwa watendaji wote wanapaswa kujiepusha na lugha zisizofaa na badala yake kuzingatia huduma bora kwa wananchi. “Kumekuwa na malalamiko katika chaguzi zilizopita juu ya baadhi ya watendaji kukosa nidhamu kwa watoa huduma, hatutegemei hilo litajirudia kwa kuwa ninyi mmepikwa vyema kwa dozi ya nadharia na vitendo,” amesema.
Vilevile, amesisitiza umuhimu wa kutoa kipaumbele kwa makundi maalum katika mchakato wa uchaguzi, akibainisha kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa Sera ya Jinsia na Ushirikishwaji wa Makundi Maalum ya Kijamii ya mwaka 2015.
Akihitimisha hotuba yake, Kamishna Awadh amewataka maafisa wote kuzingatia sheria, kutumia nyenzo walizopewa na kuendeleza amani na utulivu uliopo nchini.
Kwa upande wake Mkurungezi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi, Thabit Idarous Faina, ameahidi kwamba wataendesha uchaguzi huru, haki na salama kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Naye Msaidizi Ofisa wa Uchaguzi Wilaya ya Kaskazini B, Maryam Majid Suleiman, amesema mafunzo hayo yamewaandaa vyema washiriki na kuongeza uelewa wa pamoja katika utekelezaji wa majukumu. “Tumejengewa uwezo mkubwa wa kiutendaji, tumeelimishwa kuhusu weledi, nidhamu na jinsi ya kutoa huduma bila upendeleo. Hii itatusaidia kuhakikisha kila mwenye haki ya kupiga kura anashiriki bila vikwazo,” amesema.
Aidha amewasisitiza watendaji kufuata ngazi zote za uwajibikaji katika kutoa maamuzi ili kuwe na mfumo mzuri wa mawasiliano na upatikanaji wa Taarifa za kiutendaji.