Ussi: Walimu, madaktari waheshimiwe kazi yao ngumu

Musoma. Watanzania wametakiwa kuwaheshimu na kuwathamini walimu na madaktari nchini kwa maelezo kuwa kazi zao ni ngumu pia zinahitaji moyo wa upendo, utu, uzalendo na kujitolea ili kutimiza wajibu na majukumu yao.

Wito huo umetolewa mjini Musoma leo Jumapili Agosti 17,2025 na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa, Ismail Ussi wakati wa uzinduzi wa majengo ya kutolea huduma za kitabibu katika Hospitali ya Manispaa ya Musoma.

Ussi amesema madaktari na walimu wana majukumu magumu na makubwa katika maisha na ustawi wa jamii hivyo wanahitaji kuheshimiwa, kuthaminiwa na kutiwa moyo ili waweze kuendelea kutoa huduma stahiki kwa jamii.

“Hapa kati yetu tukisema tumchukue mtu yeyote tumpe kazi isiyokuwa ya kitaalamu mfano ya kuongoza wagonjwa kila siku kuwaelekeza chumba cha daktari na cha sindano hakika huyo mtu hatamaliza wiki hapa lazima ataacha kazi, hii inaonyesha namna gani ndugu zetu hawa wana kazi ngumu na yenye kuhitaji moyo wa kujituma na kujitolea,” amesema

Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa watumishi wa kada hizo pale wanapofika kwao kupata huduma badala ya kuanzisha ugomvi usiokuwa na sababu, huku akiwataka walimu na madaktari kutoa huduma zao kwa kuzingatia maadili na weledi.

Awali akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa majengo matatu hospitalini hapo, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Emmanuel Shani amesema Serikali ilitoa zaidi ya Sh800 milioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la dharura, meno na duka la dawa.

“Mradi umekamilika na tayari umeanza kutoa huduma ambapo faida ya mradi huu ni pamoja na kusogeza huduma karibu na wananchi mfano huduma ya kinywa na meno hivyo wananchi hawana sababu tena ya kusafiri umbali mrefu kuzifuata.

Wakati huohuo, Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (Muwasa) inatarajia kutumia zaidi ya Sh16.1 milioni kwa ajili ya kutekeleza mradi wa upandaji miti ‘rafiki wa maji’.

Kiasi hicho cha fedha kinachotokana na mapato ya ndani ya mamlaka hiyo kinatarajiwa kutumika kupanda miti katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya kwenye mradi mkubwa wa maji uliopo jirani na Ziwa Victoria katika eneo la Bukanga Manispaa ya Musoma kwa kushirikiana na jamii.

Akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Mkurugenzi Mtendaji wa Muwasa, Nicas Mugisha amesema mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2026

“Tunatarajia kupanda miti 6,000 na hadi sasa tumepanda miti 5,000 ambapo asilimia 87 ya miti iliyopandwa inaendelea vizuri, lengo letu ni kuhakikisha pamoja na mambo mengine tunalinda na kudumisha rasilimali za maji kwa njia endelevu,”amesema.

Akizungumza baada ya kupanda mti kwenye mradi huo, Kiongozi huyo wa mbio za mwenge, mbali na kupongeza mamlaka hiyo kwa mradi huo pia amesema ipo haja ya jamii nzima kushirikiana kwa pamoja katika kuhifadhi vyanzo vya maji nchini.

“Vyanzo vingi vya maji vipo karibu na jamii na vinaathirika na shughuli za kujamii hivyo suala la kuvitunza ni jukumu letu sote ili miradi ya maji ambayo inatekelezwa na Serikali kwa gharama kubwa iweze kudumu na kuwanufaisha wananchi vizazi na vizazi,” amesema Ussi.