Arusha. Wadau mbalimbali wa kilimo ikolojia wamekutana jiji Arusha kujadiliana biashara ya mipakani ya mazao ya kilimo ikolojia ili kuainisha changamoto na kuangalia namna ya kukabiliana nazo ili kukuza kilimo hicho.
Wadau hao kutoka wizara mbalimbali hapa nchini, sekta binafsi na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wamekutana kuangalia namna ya
kusimamia biashara za kikanda ikiwamo kuratibiwa vizuri na kuwa na manufaa kwa wazalishaji.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika leo Agosti 17, 2025, Mratibu wa Shirika la Wakulima Tanzania (Shiwakuta), Richard Masandika amesema kabla ya kukutana utafiti ulifanyika katika mipaka ya Tanzania, Kenya na Rwanda ambayo ni Namanga, Tarakea na Rusumo, umeonyesha kuwepo kwa mfumuko mkubwa wa biashara za kilimo ikolojia. Amesema miongoni mwa changamoto walizobaini ni pamoja na wazalishaji wengi kutozingatia ubora wa bidhaa.
Kutokana na sababu hiyo, amesema wao kama wadau wanapaswa kujenga uelewa wa viwango kwa wazalishaji na wachakataji ili kuboresha bidhaa zao na kuweza kushindana katika masoko ya kikanda.
“Utafiti unaonyesha Tanzania tunapeleka mazao mengi ya nafaka Kenya na Rwanda, lakini kuna baadhi ya bidhaa zinachakatwa Kenya na kuja Tanzania, hii inaonyesha Tanzania tunapaswa kufanya kazi ya ziada ili kuchakata bidhaa zetu kuongeza ubora zinaposafirishwa nje ya nchi.”
Awali, mchambuzi wa sera kutoka shirika lisilo la kiserikali la Alliance for Food Sovereignty in Africa (AFSA), Africa Kiiza amesema utafiti huo uliofanyika hivi karibuni unaonyesha kuna changamoto zinazokwamisha bidhaa hizo kuuzwa katika masoko ya kikanda licha ya kuwepo kwa sera mbalimbali.
Kiiza amesema wameamua kuanza kufanya majadiliano na Serikali, watunga sera na EAC, kuona njia ya kuwezesha bidhaa kufikia masoko bila changamoto.
“Mazao ya kilimo ikolojia ni yale yanayozalishwa kwa kutumia mbolea za asili, hakitumii kemikali kali. Tunaona lazima tuweke njia za kupunguza vikwazo ili kuwezesha wakulima wafikie masoko hayo,” amesema.
Amesema AFSA, kwa kushirikiana na wadau wengine, itaendelea kuwajengea uwezo wadau mbalimbali, ikiwemo wafanyabiashara wa mazao hayo.
Akiwasilisha mapendekezo ya kisera kutokana na warsha hiyo, Ofisa wa Utetezi na Ushawishi wa Shiwakuta, Thomas Laizer ametaja miongoni mwa mapendekezo hayo ni Serikali za EAC kuondoa vikwazo vya mazao hayo mipakani ambavyo vinaathiri biashara, viwango vya ubora wa bidhaa na udhibiti wa bidhaa zisizo na ubora.
Laizer amesema wamekubaliana ni muhimu kuchukuliwa kwa hatua madhubuti kuondoa au kupunguza vikwazo visivyo vya kikodi ikiwemo mazuio yasiyo rasmi ya barabarani ambayo kwa kiasi kikubwa yanaathiri biashara za mipakani.
Amesema vikwazo hivyo vinaumiza wakulima kwani baadhi ya wafanyabiashara huishia kununua mazao kwa bei ya chini kufidia hasara wanayoitarajia kukumbana nayo wasafirishapo mazao.
Laizer ametaja mapendekezo mengine ni Serikali na wadau, kuchukua hatua ya kuwekeza katika kuwaelimisha wakulima kuhusu mahitaji ya kisera na kisheria yanayohusu uzalishaji wa mazao na bidhaa za kilimo ikolojia, ili washiriki kikamilifu katika biashara za mipakani na kukuza uchumi wa kilimo endelevu.
Mmoja wa wakulima wa kilimo ikolojia kutoka wilayani Karatu, George Ndege amesema miongoni mwa faida za kilimo hicho ni pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula, inapunguza gharama kwa mkulima na matumizi ya mbolea na viuatilifu vya asili.