Namtumbo. Wakulima wa zao la tumbaku kupitia Chama cha Msingi Namkeke, wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, wameanza kufufua kilimo hicho baada ya kupata mnunuzi mpya anayenunua tumbaku kwa bei nzuri na kulipa kwa wakati.
Hatua hiyo imeleta matumaini mapya kwa wakulima waliokuwa wamesitisha uzalishaji kwa muda mrefu kutokana na changamoto mbalimbali.
Kupitia ushirikiano huo, wakulima wameanza kunufaika kiuchumi kwa kutumia mapato ya tumbaku kuboresha maisha yao.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Namkeke, Casberth Nchimbi amesema alipoteuliwa kuongoza chama hicho alikuta wanachama wanane waliokuwa wakilima tani sita pekee za tumbaku.
Nchimbi amesema wakulima wengi walikuwa wamekata tamaa kutokana na changamoto nyingi zilizokikumba kilimo hicho.
Hata hivyo, amesema msimu wa 2024/2025 wanachama wameongezeka na kufikia 55, huku matarajio yakiwa ni kufikia wanachama 100 msimu wa 2025/2026, kutokana na mvuto wa huduma bora zinazotolewa na kampuni ya 3H TOBACCO LTD.
Aidha, Nchimbi ameishukuru kampuni hiyo kwa ushirikiano mzuri na huduma bora kwa wakulima, ambazo amesema zimechangia kuinua uchumi wa wananchi wa chini waliokuwa wamesusia kilimo hicho kwa muda mrefu.
Nchimbi amezitaka kampuni nyingine za ununuzi wa tumbaku kuiga mfano wa kampuni hiyo kwa kuwajibika na kushirikiana kikamilifu na wakulima ili kuinua maisha yao.
Mmoja wa wakulima hao, Abdallah Ndine amesema tumbaku imemuondoa kwenye umaskini kwani alikuwa akidharauliwa na wenzake kutokana na dhiki aliyonayo kwa muda mrefu, lakini tangu alipofika mfadhili huyo ambaye anawakopesha pembejeo na kuwalipa kwa wakati maisha yake na familia yamebadilika.
“Baada ya kuuza tumbaku yangu na kulipwa kwa wakati, niliweza kununua usafiri nikafanikiwa kununua pikipiki ambayo sasa inamuingizia kipato cha ziada,” amesema Ndine.

Kwa upande wake, Meneja wa kampuni hiyo, Issa Ponera amesema imejipanga kuhakikisha inaendelea kumuwezesha mkulima kwa kumlipa fedha zake kwa wakati na pia kumsafirishia mazao yake kutoka shambani, hatua ambayo imepunguza gharama kubwa ambazo wakulima walikuwa wakizikabili awali.
Amesema, sera nzuri zilizowekwa na Serikali zimesaidia kuboresha zao hilo ambapo tayari wameshalipa wakulima chama hicho zaidi ya Sh266 milioni na bado inaendelea kulipa.