Arusha. Taharuki imeibuka kwa wananchi kufuatia mpango wa kuanzishwa mradi mpya wa uchimbaji magadi soda ndani ya Ziwa Natron lililohifadhiwa kutokana na upekee wake duniani wa kuwa mazalia ya ndege aina ya flamingo.
Mpango huo unaotaka kutekelezwa na Kampuni ya Ngaresero Valley, ambapo inadaiwa kutaka kujengwa kiwanda cha kuchakata magadi soda kandokando ya ziwa hilo, jambo lililoibua taharuki kwa wananchi wa vijiji tisa vinaolizunguka ziwa.
Kufuatia taarifa hizo, viongozi wa serikali ya vijiji na viongozi wa mila kwa pamoja waliitisha mkutano wa dharura kujadili mpango huo na kuibuka na kauli moja ya kuupinga wakisema; mradi huo ni tishio kwa mazingira asilia ya ziwa, mifugo, kilimo na hata uchumi wao kupitia mapato ya watalii wanaotembelea eneo hilo.
Katika kikao hicho kilichokutanisha wazee wa mila na viongozi wa vijiji vya Engaresero, Pinyinyi, Gelai Lumbwa, Ichangiti Sapukin, Alaililai na Wosiwosi (Ngorongoro), pamoja na Magadini, Loondolwa Esirwa na Gelai Merugoi (Longido) vilivyopo jijini Arusha.
Akizungumza katika kikao hicho, mwenyekiti wa baraza la wenyeviti wa vijiji hivyo tisa vinavyozunguka Ziwa Natroni, Joshua Muriatoi Mollel amesema kuwa mradi huo ni tishio kubwa la uhai wa ziwa hilo lililohifadhiwa miaka mingi kwa ajili ya utunzaji wa mazingira, asilia ya eneo na zaidi kwa ustawi wa shughuli zao za kilimo na mifugo na utalii.
“Si mara ya kwanza kampuni mbalimbali kufanya majaribio ya kuchimba magadi soda hapa hii ni zaidi ya mara tatu ikiwemo mwaka 2008 kampuni ya Tata Chemical kutoka India na hata Serikali mwaka 2022 lakini tulisimama na msimamo huu na wakaondoka.
“Hivyo kwa sasa tunaomba Serikali tena isimame na sisi kutunza ziwa hili ambalo ni eneo pekee la mazalia ya ndege aina ya Flamingo Afrika Mashariki, na zaidi ndio tegemeo la ndege hao duniani ambao wako hatarini kutoweka,” amesema.
Mwenyekiti wa Engaresero, James Sapuro Lywangiri amesema faida kubwa wanayopata wao katika ziwa hilo mbali na kuwa sababu ya mito midogo inayosaidia mifugo kunywa maji na kilimo cha umwagiliaji, lakini pia wanafaidika na mapato ya utalii.
“Watalii wengi wanakuja kutembelea ziwa hili kujionea ndege aina ya flamingo kutokana na zaidi ya asilimia 80 duniani wapo hapa, na wengine wanakuja kufanya utafiti lakini pia mafunzo ya vitendo na hivyo kulipa mapato ambayo yanasaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa zahanati, shule na hata miundombinu ya maji,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya shirika lisilo la kiserikali la Engaresero Emairete Community Development Initiative (EECDI) linalosimamia vivutio vya utalii katika eneo hilo, Daniel Sironga amesema kuwa kupitia vivutio vya utalii katika eneo hilo ikiwemo Oldonyo lengai (Mlima wa Mungu) na Ziwa Natron wamefanikiwa kuajiri zaidi ya waongoza watalii 109.
“Hili ziwa likifa zaidi ya watu 180 watakosa ajira wakiwamo waongoza watalii 109 ambao wanatembeza watalii katika ziwa hilo wanaokuja kujionea ndege, kupiga picha na zaidi wengine wanakuja kufanya utafiti na masomo kwa vitendo,” amesema.
Mwenyekiti wa Kijiji cha, Loondolwo, Keton Ngairugoi, amewataka wawekezaji wanaotaka kufanya miradi ya magadi soda kuelekeza nguvu zao katika eneo lililoanzishwa na Serikali lililopo kijiji cha Engaruka wilayani Monduli.
Mzee wa kimila wa Kijiji cha Wosiwosi, Meihaa Laiseri amesema kwa mujibu wa mwekezaji aliyefanya utafiti anahitaji zaidi ya zaidi ya hekta 45,000 kwa ajili ya mradi huo, zikiwemo pampu, mabomba na kiwanda kikubwa cha kusafisha magadi soda.
“Hatuna ardhi kubwa kiasi hicho iliyo wazi, labda wanataka kuwatimua wananchi wetu waanze kutangatanga na kuwa wakimbizi katika maeneo ya wengine, hivyo tumeona mradi pia utaangamiza maisha yetu na urithi wa Taifa,” amesema.
Kwa upande wake mwekezaji wa mradi huo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ngarasero Valley, Khalid Abdalah Rashid amesema kuwa wameshafanya utafiti na wanatarajia kuanza mradi baada ya kukamilisha taratibu za vibali na leseni.
“Mradi huu bado haujaanza lakini utaanza mara moja baada ya kukamilisha taratibu za vibali, na utazalisha zaidi ya tani 660 za magadi soda kwa mwaka na kutoa ajira za kutosha kwa wananchi.
“Hatuna nia mbaya na mazingira na wananchi wa eneo lile maana tuliongea na baadhi yao na wamekubali na uzuri kiwanda kitatoa ajira pia kwao,“ amesema.
Wakati mwekezaji huyo alisema hayo, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Kanali Wilson Sakulo amesema kuwa hawana taarifa za mradi huo na hauwezi kutekelezwa ndani ya ziwa.
“Hizo taarifa bado sijapata nazisikia tu, lakini hazijaja kwangu rasmi hivyo jueni tu kuwa hakuna mradi kama huo Ziwa Natron,” amesema.
Mtaalamu wa maswala ya ndege kutoka shirikisho la kimataifa la uhifadhi wa mazingira (IUCN) aliyebobea katika utafiti wa flamingo, Emmanuel Mgimwa amesema kuwa uwekezaji wowote ndani ya ziwa hilo utazidisha hatari ya kutoweka kwa ndege hao.
Amesema kuwa Tanzania ina zaidi ya asilimia 80 ya ndege aina ya flamingo duniani ambao wamebakia, wengi wametoweka kutokana na kuharibiwa kwa mazingira yao ya kuishi na mazalia yao.
“Ukiangalia duniani kwa sasa flamingo wamepungua sana na wako kati ya milioni 1.5 hadi milioni mbili, wakati miaka minne hadi mitano nyuma walikuwa zaidi ya milioni 4.5 hadi tano, na hii imetokana na mazalia yao kuharibiwa,” amesema Mgimwa ambae pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Nature Tanzania inayotetea maisha ya ndege nchini.
Amesema uchimbaji wa magadi utahitaji kufyonza maji mengi kutoka ziwani na hata kubadilisha mtiririko wa mito muhimu, ikiwemo Mto Ewaso Ng’iro kutoka Kenya, jambo litakalosababisha kuvurugika kwa usawa wa maji na kuhatarisha kabisa uzalishaji wa flamingo.
Aidha Ziwa Natron limepewa hadhi ya kimataifa kupitia Mkataba wa Ramsar, likiwa kimbilio la ndege zaidi ya 100,000 wa maji na samaki adimu Oreochromis alcalicus, pamoja na mwani aina ya spirulina platensis unaolisha flamingo.