Si mara ya kwanza wala ya mwisho kujadili mauaji na ukatili dhidi ya kinamama na watoto kutokana na kutoelewana katika ndoa.
Japo hakuna habari nzuri, mauaji ya watoto na wanandoa yatokanayo na kutoelewana kwa wanandoa yanazidi kushamiri nchini.
Mauaji ya namna hii yamekuwa matukio ya kawaida yanayoripotiwa na vyombo vyetu vya habari hata vya nje ya nchi.
Vyanzo vikubwa vya jinai hii inayozidi kushamiri na kupoteza maisha ya watu wengi tena wasio na hatia husababishwa na vitu kadhaa.
Mojawapo ya visababishi ni ukosefu wa uaminifu katika ndoa, changamoto ya afya ya akili, ujinga, ukatili dhidi ya kinamama na watoto, uzinzi, na kukosekana au kuzidi kuporomoka kwa maadili ya kindoa.
Kwa mfano, takwimu za mwaka 2019 za Jeshi la Polisi nchini zilitaarifu kuwa wanaume 750 waliua wake zao na 74 kati yao wamejiua huku wanawake 158 wakiua waume zao na 39 kati yao kujiua.
Mwaka 2020 waume walioua wake zao ni 226 na kati yao waliojiua baada ya kuua ni 30, huku wanawake walioua waume zao ni 71 na kati yao 12 walijiua baada ya kuua waume zao. Wimbi la mauaji ya wanandoa liliendelea.
Mwaka 2021 (hadi Septemba 30) waume walioua wake zao ni 156 na kati yao waliojiua baada ya kuua ni 16, ilhali wanawake walioua waume zao ni 29 na kati yao tisa walijiua baada ya kuua waume zao.
Duniani kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa, asilimia 40 ya vifo vya wanawake duniani, asilimia sita hutokana na vifo visababishwavyo na wenza wa wanandoa.
Wapo wanaoua watoto kwa sababu za kubambikiwa na wenza wao kadhia ambayo imeshamiri na hasa baada ya kugundulika kipimo cha DNA kinachoshughulika na vinasaba.
Pia, wapo wanaoua kinamama na kuwaacha watoto wakati pia wapo wanaoua wote ukiachia mbali wanaoua wote nao wakijimaliza.
Kinamama acheni jinai na mchezo huu, ambavyo licha ya kuwaumiza, pia huumiza watoto wenu wasio na hatia.
Japo si rahisi kuvaa viatu vya watenda na watendewa, hatujui kama kuna binadamu mwenye haki ya kuutoa uhai wa mwingine hata angekosewa vipi hasa ikizingatiwa kuwa sifa mojawapo ya binadamu ni kukosa na kukosea.
Kuna masuala na maswali ya lazima na muhimu tunayopaswa kuhangaishwa nayo, ili tuweze kushinda na kuondoa kadhia hii, inayoelekea kuwa janga kwa binadamu wengi wasio na hatia ambao ni tegemeo la kesho kwa kila jamii.
Hivi Mungu angeamua kutuhukumu, wangapi wangeendelea kuishi na kufaidi mema yake? Unauaje kiumbe au viumbe ambao huwezi kuumba?
Je, wanapowaza kuwaua watoto huwa wanajiuliza kuwa kama wangekuwa waathirika, wangefanya au kutaka kufanyiwa nini?
Tuzidi kujiuliza zaidi. Hivi watoto huwa na makosa gani au mchango katika jinai hii zaidi ya kuwa waathirika na matokeo ya visababishi tajwa hapo juu? Je, wauaji au wale wanaopanga kufanya hivyo, waliwahi kujiuliza wangekuwa wapi kama wazazi wao wangekuwa katili na ovyo kama wao?
Hii inatoa picha gani kwa watoto kwa ujumla? Kwani hakuna namna nyingine ya kutatua matatizo yenu hata kuadhibiana ikibidi zaidi ya ukatili na mauaji dhidi ya watu wasio na hatia?
Wanapowaua au kuwatesa waathirika, wanapata nini zaidi ya kuongeza uzito na ugumu wa tatizo?
Japo wahusika wanaweza kujitetea, kuhadaa wengine au kujiridhisha hata kujidanganya na kujipa imani bandia kuwa wanafanya mauaji na ukatili dhidi ya kina mama na watoto kutokana na kuudhiwa, hawana sababu zozote za msingi kufanya hivyo.
Tuhitimishe kwa kushauri kinababa wanaogundua jinai kama hii, watulize akili zao na kuvaa viatu vya waathirika.
Kama wakifanya hivi, hamna haja ya kuwaua watoto wasio na hatia hata hao waliowabambikizia. Cha msingi ni kuachana nao salama na kuanza maisha upya pamoja na kuumizwa sana.
Pia, ni vizuri kukumbuka kuwa wakati mkipendana hao watoto hawakuwapo wala hawakushiriki zaidi ya kuwa matokeo ya kazi yenu.