Shinyanga. Chifu Inspekta wa mgodi unaomilikiwa na Kikundi cha Wachapakazi, Fikiri Mnwagi, amethibitisha kuopolewa kwa miili ya watu wawili waliopoteza maisha kwenye ajali ya mgodi iliyotokea katika kijiji cha Mwongozo, Kata ya Mwenge, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Akizungumza leo Agosti 17, 2025, na waandishi wa habari akiwa eneo la tukio, Mnwagi amesema shughuli ya uokoaji inaendelea vizuri, ambapo wote waliokuwa kwenye duara namba 106 wamekwishatolewa, watatu wakiwa hai na watatu wakiwa wamefariki dunia.
“Leo tumeopoa watu wawili wakiwa wamefariki dunia. Kwa sasa tumebakiza duara namba 20 lenye watu wanane, na duara namba 103 lenye watu 10.
“Mmoja alitolewa akiwa amefariki. Tunatarajia kukamilisha shughuli hii ndani ya siku mbili au tatu zijazo,” amesema Mnwagi.
Jana Agosti 16, 2025 Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro alisema watu wawili wamegundulika eneo walipo ardhini, lakini juhudi za kuwatoa zilikumbana na vizuizi vya mawe ambapo waokoaji walipata wakati mgumu kuwafikia kwa wakati.
Ajali hiyo ilitokea Agosti 11, 2025 wakati maduara ya mgodi huo yakiwa yanafanyiwa ukarabati na kupelekea mgodi kutitia na kufukia watu 25, Agosti 12, 2025 watu watatu waliokolewa wakiwa hai na kupelekwa hospitalini. Wawili wameruhusiwa lakini mmoja alipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.
Pia, Agosti 13, 2025 mtu mmoja aliokolewa akiwa majeruhi alipelekwa hospitalini, lakini juhudi za madaktari hazikufua dafu alifariki dunia wakati anapatiwa matibabu, juhudi za kuokoa ziliendelea na Agosti 15 mwili wa mtu mmoja uliopolewa na kutambulika kwa jina Mgunda Ng’ondi (28).
Hadi sasa watu saba wametolewa huku watatu wakiwa hai na wanne wakiwa wamefariki, juhudi za kuwatoa wengine 18 zinaendelea kwa kasi kwa kutumia mashine za utambuzi wa ardhini.
Hata hivyo, baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wa waliofukiwa mgodi akiwemo Joseph Buzuka mwenye vijana wawili waliofukiwa na Monica Andrea mwenye kaka wanne waliofukiwa wamekuwa wakisubiri hatima ya ndugu zao, huku tumaini la kuwaona wakiwa hai likipotea siku hadi siku.
Serikali haikuwa mbali na waathirika ambapo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo wamefika eneo la tukio na kutoa salamu za pole kwa waathirika na kuahidi kuwapa mahitaji yote muhimu kwa ndugu waliotoka maeneo ya mbali wakati wakisubiri ndugu zao.