KIKOSI cha Tanzania Prisons kinaendelea na maandalizi ya msimu ujao, huku kikivuta pia mastaa wapya kimyakimya ambapo kwa sasa kipo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa winga wa JKU ya Zanzibar, Neva Kaboma.
Awali, mchezaji huyo ilidaiwa angejiunga na Coastal Union ambayo mwanzoni ilifanya mawasiliano na waajiri wake ingawa moja ya changamoto iliyojitokeza ni mabosi wa kikosi hicho kushindwa kutoa fedha mapema na JKU kufanya biashara na Prisons.
Taarifa ambazo Mwanaspoti limezipata zinaeleza Prisons imemalizana na uongozi wa JKU na sasa nyota huyo amepewa ruhusa ya kukubaliana suala la maslahi binafsi licha ya uhusiano wake mzuri na Coastal Union tangu michuano ya Muungano.
Coastal Union ilianza kumfuatia nyota huyo tangu michuano ya Muungano iliyofanyika mwaka huu Zanzibar, ambapo mabosi wa kikosi hicho walimuahidi wangemsajili msimu wa 2025-2026, ingawa suala la fedha limekuwa changamoto kwao.
Kutokana na JKU kucheleweshewa kuingiziwa fedha na Coastal Union huku Prisons ikiwa mstari wa mbele, mabosi wa timu hiyo wamekubaliana kila kitu hivyo kwa sasa kinachosubiriwa ni maslahi binafsi ya mchezaji mwenyewe ili asaini mkataba.
“Mkataba na Tanzania Prisons ni wa mwaka mmoja ila mwenye kipengele cha kuongeza mwingine. Suala la maslahi sio tatizo kubwa kwa sababu mchezaji mwenyewe ameonyesha utayari japo ana uhusiano mzuri na Coastal Union,” kilisema chanzo hicho.
Nyota huyo aliyezaliwa Februari 15, 2001 ana uwezo wa kucheza winga ya kulia na kushoto, huku msimu wa 2024-2025 akihusika na mabao 19 ya JKU katika Ligi Kuu Zanzibar baada ya kufunga saba na kuasisti 12.