Dar es Salaam. Zaka imetajwa kuwa ni miongoni mwa nyenzo muhimu za kupunguza umaskini nchini kupitia uwezeshaji wa mitaji kwa wananchi wanaohitaji kuanzisha shughuli za kiuchumi.
Kauli hiyo imetolewa na Sheikh Ibrahim Ghulam, Mwenyekiti wa Bodi ya Baytul-Mal (Mfuko wa Zaka), katika hafla ya ugawaji msaada wa zaka kwa walengwa 20 jijini Dar es Salaam. Walengwa hao walijumuisha akina mama waliokosa mitaji, wanafunzi waliokwama kulipia ada, wagonjwa, wenye madeni na watu wenye ulemavu.
Sheikh Ghulam amesema mfuko huo unachangia juhudi za Serikali na wadau wengine katika kupunguza umaskini, hususan kwa kuwezesha wananchi kujitegemea. Alikumbusha historia ya Uislamu ambapo zaka iliposimamiwa kwa uadilifu katika zama za Khalifa Umar bin Abdulaziz, ilitosheleza mahitaji ya jamii yote na hata kupelekwa katika maeneo mengine.
Baytul-Mal ilianzishwa mwaka 2002 ili kuweka utaratibu wa utekelezaji wa ibada hiyo kwa kuanzisha mfumo rasmi wa ukusanyaji na ugawaji. “Tuliona kuna utaratibu usio rasmi katika kugawa zaka, ndio maana tukaona tuunde chombo kitakachokusanya na kuzigawa kwa uwazi na uadilifu,” amesema Sheikh Ghulam.
Hata hivyo, ameeleza kuwa changamoto kubwa ni uwezo mdogo wa kuwafikia wanaowajibika kutoa zaka, jambo linalopelekea ombi kuwa kubwa zaidi kuliko rasilimali zilizopo.
Kwa upande wake, Katibu wa Bodi ya Baytul-Mal, Haji Mrisho Rubibi, amesema zaka ni nguzo ya nne katika Uislamu inayolenga kujenga nguvu za kiuchumi za jamii nzima. Amebainisha kuwa dhana ya zaka inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025–2050 ambayo inalenga kujenga uchumi imara, shindani na jumuishi.
“Kwa kuwajengea uwezo Watanzania na kuwasaidia walengwa wa zaka, tunaendana na dira ya Taifa. Leo tumewapatia watu 20 kila mmoja Sh500,000, na mwaka huu idadi ya waliopata msaada huu imefikia 50,” amesema Rubibi.
Amefafanua kuwa fedha hizo hazina masharti yoyote na baadhi ya walengwa walipatiwa mafunzo ya usimamizi wa biashara kabla ya kuanza shughuli zao. Waliofaidika ni pamoja na walemavu wa macho, wazazi wa watoto wenye maradhi sugu na wajasiriamali wadogo wanaoanza biashara.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mwanakheri Omari Abdallah wa Mwananyamala amesema msaada huo ni mwanga mpya utakaosaidia kubadilisha maisha yao.
Shughuli za Baytul-Mal, zinazosimamiwa na Jumuiya ya Wataalamu wa Kiislamu Tanzania (Tampro) na Umoja wa Wanazuoni Tanzania (Hay-atul Ulamaa), zimekuwa zikifanyika kwa weledi na uadilifu, na hadi sasa mfuko huo umesaidia mamia ya wananchi nchini.